Windows

DC Ngubiagai awatahadharisha wanaojenga ndani ya hifadhi ya barabara


Na Ahmad Mmow, Lindi

Wananchi wilayani Kilwa, mkoani Lindi wametahadharishwa wasijenge nyumba ndani ya hifadhi za barabara.

Wito huo ulitolewa jana na mkuu wa wilaya hiyo, Christopher Ngubiagai alipozungumza na wananchi wa kijiji cha Makangaga, kilichopo wilayani humo.

Ngubiagai ambae yupo katika ziara ya kikazi katika vijiji vya wilaya hiyo, alisema ili kuepuka malalamiko na hasara, wananchi hawanabudi kuheshimu sheria. Ikiwemo kutojenga ndani ya hifadhi za barabara kama sheria inavyotaka.

Alisema wananchi hawana sababu za kujenga ndani ya hifadhi wakati wakala wa barabara nchini( TANROADS) umeweka alama kubwa zinazoonesha mwisho wa upana wa barabara.

''Barabara hii ( Kiranjeranje-Makangaga- Nanjirinji-Ruangwa) ni ya serikali, ipo kwenye mpango wa kujengwa kwa kiwango cha lami. Kwahiyo msijenge kwenye hifadhi ya barabara,'' alisisitiza Ngubiagai.

Aidha mkuu huyo wa wilaya ya Kilwa ambae alitoa tahadhari hiyo baada ya wananchi kumlalamikia ubovu wa barabara hiyo, alisema kukamilika kwa ujenzi wa barabara hiyo kutafungua fursa za uchumi kwa wananchi hao.

Post a Comment

0 Comments