YANGA kwa sasa imekuwa dili miongoni mwa wachezaji waliong’ara msimu huu kutoka ndani na nje ya Tanzania, wakivutiwa na mamilioni yaliyopo Jangwani ya usajili.
Baada ya msimu uliomalizika mapema wiki hii Yanga kuambulia patupu, imetangaza kufanya usajili wa kutisha, ikiringia fedha walizonazo zinazotajwa kufikia milioni mbili.
Tayari Wanajangwani hao wameanza kushusha ‘mashine’ kadhaa kutoka ndani na nje ya Tanzania, ikielezwa kuwa watano wameshamwaga wino.
Baadhi ya wachezaji ambao wanatajwa kusaini mkataba Yanga hadi jana ni mawinga wawili matata kutoka Rwanda, Patrick Sibomana na Issa Bigirimana, beki Mghana Lamine Moro na kiungo Abdulazizi Makame kutoka Zanzibar.
Wengine ni straika kutoka Zambia, Winston Kalengona kipa Farouk Shikhalo wa Bandari FC ya Kenya, ambao kila mmoja amepewa mkataba wa miaka miwili.
Akizungumzia usajili wao, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela, amewahakikishia mashabiki kuunda kikosi cha nguvu cha msimu ujao.
Alisema usajili wao umelenga kuboresha kikosi hicho ambacho kwa msimu wa pili mfululizo kimeambulia patupu na kuwaacha mahasimu wao wa jadi, Simba, wakijinafasi kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mwakalebela alisema bado hawajamaliza usajili wao na kinachowasubirisha kwa sasa ni fedha ambazo wanatarajia kuzipata Juni 15, mwaka huu.
Alisema Juni 15 watafanya harambee ya kukusanya fedha iliyopewa jina la Kubwa Kuliko ambapo kiasi chote watakachokusanywa kitaelekezwa katika usajili.
“Mpaka sasa tumeshasajili wachezaji sita, tunasubiri tumalize harambee ya Kubwa Kuliko tuendelee na usajili,” alisema.
Wakati huo huo, meneja wa wachezaji nyota wa Simba (jina kapuni), ameonekana kuweweseka na ‘burungutu’ la usajili walilonalo Yanga na hivyo kuanza mchakato wa chini kwa chini kuwauzia vifaa Wanajangwani hao.
Mmoja wa rafiki wa karibu na meneja huyo, ameliambia BINGWA: “(Anamtaja jina), ana usongo na Yanga, anatamani sana kuwaletea wachezaji akiamini huko watapata nafasi ya kucheza kuliko Simba, lakini pia kwa kuwa Yanga ni timu kubwa.
“Lakini anashindwa kujitokeza hadharani kwa kuwa Simba hawatamwelewa, ila kuna uwezekano wa kufanya biashara na Yanga kwa kuwa anajua msimu huu wa pesa (fedha) tofauti na ilivyokuwa msimu uliopita.
0 Comments