Esperance ya Tunisia usiku wa kuamkia leo ilitetea taji la ligi ya mabingwa barani Afrika baada ya kuichapa Wydad Casablanca bao 1-0 katika mchezo ambao ulivunjika, Casablanca wakigoma kucheza baada ya mwamuzi kukataa bao lao
Esperance wameibuka mabingwa kwa ushindi wa jumla wa mabao 2-1. Katika mchezo kwanza uliofanyika nchini Morocco timu hizo zilitoka sara ya bao 1-1
Katika mchezo huo uliosimama kwa karibu saa moja, Esperance ilipata bao la kuongoza kwenye kipindi cha kwanza likiwekwa kimiani na Youcel Belaili
Kwenye dakika ya 59 Walid El Karti akaisawazishia Wydad lakini bao hilo likakataliwa na mshika kibendera kuwa Karti alikuwa ameotea
Hata hivyo picha za marudio za televisheni zilionyesha dhahiri kuwa mfungaji hakuwa ameotea
Utata zaidi ni kuwa mfumo wa VAR ambao ulipaswa kutumika kama ilivyokuwa katika mchezo wa kwanza, haukuwa ukifanya kazi
Wydad waligoma kuendelea na mchezo huo wakitaka mwamuzi aende akajiridhishe na picha za marudio za VAR lakini ikawa haifanyi kazi
Hapo ndipo Wydad walipogoma kuendelea na mchezo wakiamini walikuwa wakihujumiwa
Baada ya mwamuzi kuwataka warejee uwanjani baada ya majadiliano ya muda mrefu, bado wakagoma hivyo kuamua kumaliza mchezo
Nahodha wa Esperance Khalil Chemmam aliwaambia waandishi wa habari kuwa kabla ya mchezo mwamuzi aliwataarifu manahodha wa timu zote kuwa hakutakuwa na VAR lakini anadhani nahodha wa Wydad hafahamu lugha ya Kifaransa
0 Comments