MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugezi ya Simba, Mohammed Dewji `Mo`, amewataka wapenzi wa klabu hiyo kutulia juu ya tetesi za usajili wa nahodha wa Yanga, Ibrahim Ajib, akiahidi kila kitu kuwa wazi ndani ya siku chache zijazo.
Kumekuwa na taarifa kwamba Ajib ameshamalizana na Simba kwa makubaliano maalumu, huku akiwa amepewa Sh mil. 85 pamoja na gari aina ya Crown ili kurejea katika kikosi cha Wekundu wa Msimbazi hao.
Akizungumza Dar es Salaam juzi, Mo alisema mikakati yao ipo vizuri katika suala la usajili wa wachezaji wa kigeni pamoja na wale wa ndani na kwamba majina yataanikwa baada ya viongozi wa klabu hiyo kukutana na benchi la ufundi linaloongozwa na Mbelgiji, Patrick Aussems.
“Suala la usajili liko vizuri zaidi, kwani tumetenga kiasi kikubwa cha fedha, lakini pia suala la Ajib litajulikana baada ya bodi kukutana na kocha kujadili ripoti tuliyokabidhiwa na Aussems,” alisema.
Mo alisema kila kitu kinaenda vizuri, hivyo mashabiki na wadau wasiwe na mashaka juu ya usajili, kwani watazingatia mapendekezo watakayopewa na kocha wao huyo.
Kikosi cha Simba kimefanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ikiwa ni pamoja na kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mafanikio hayo yametokana na usajili wa nguvu uliofanywa na klabu hiyo kwa kuwanasa wachezaji wazuri kutoka nje ya Tanzania na wale wa ndani.
Miongoni mwa wachezaji walioipaisha Simba msimu huu ni Aishi Manula, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Haruna Niyonzima, Clatous Chama, James Kotei, Emmanuel Okwi, Meddie Kagere, Muzamiru Yassin, Asante Kwasi, Nicholas Gyan, nahodha John Bocco na wengineo.
0 Comments