NYOTA ya mshambuliaji wa Simba, Meddie Kagere, imezidi kung’ara ambapo kwa sasa klabu lukuki zimeendelea kumiminika kuitaka saini yake kwa ajili ya msimu ujao.
Kagere ni miongoni mwa wachezaji waliochangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya Simba msimu huu, wakiiwezesha kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini pia timu hiyo ikifika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Katika mechi za Ligi Kuu Bara, Kagere alifunga mabao 23, yaliyomwezesha kutwaa kiatu cha dhahabu cha ufungaji bora na pia kuwa mchezaji bora wa msimu wa Simba.
Ni kutokana na makali yake hayo aliyoyaonyesha akiwa na kikosi chake cha Simba, klabu mbalimbali zimeonekana kuvutiwa naye ili kunufaika na huduma yake.
Akizungumza na BINGWA jana, Meneja wa mchezaji huyo, Patrick Gakumba, alisema kuna ofa nyingi zinamiminika katika simu yake ambazo zinamhitaji Kagere.
Alisema hali hiyo inampa furaha, kwani kama ofa zinakuwa nyingi, maana yake mchezaji anafanya kazi nzuri ambayo kila mtu anaiona na kuhitaji huduma yake.
“Pamoja na ofa kuwa nyingi, mimi siwezi kufanya maamuzi kwasababu Kagere ni mali ya Simba,” alisema.
Kwa upande wake, Kagere alisema pamoja na ofa kuwa nyingi, lakini hawezi kuamua lolote, kwani maamuzi ni ya klabu yake.
Alisema mchezaji ni sawa na mfanyabiashara, kama mabosi wake watakubali kumtoa, yeye hana shida.
“Mimi naangalia faida, lakini kwa sasa nina mkataba na mabosi wangu na kama unavyoona, timu yetu inafanya vizuri.
“Kama wao wataona kuna faida ya kutosha kuniuza kwenye hizo timu, mimi siwezi kupinga maana wao ndio wenye maamuzi kwasasa,” alisema Kagere.
Katika hatua nyingine, Gakumba amesema kuwa ana orodha ya wachezaji wengi wazuri waliopo sokoni, hivyo kama kuna klabu inahitaji, yupo tayari kuwaletea vifaa vya nguvu.
“Kuna wachezaji wengi sana wazuri, kama nitaamua kuwaleta Tanzania, basi hakuna mtu ambaye atakataa kazi zao,” alisema.
0 Comments