WAKATI uongozi wa Yanga ukiwa kimya kwa baadhi ya nyota wake imebainika kuwa hata kiungo mkongwe wa timu hiyo, Haruna Moshi ‘Bobani’ bado hajapigiwa simu na bado anawasikilizia kujua hatma yake.
Boban alijiunga na Yanga kipindi cha dirisha dogo kwa mkataba wa miezi sita na sasa hivi ligi imemalizika bado hajafahamu hatma yake kwa msimu ujao.
Akizungumza na Spoti Xtra, Meneja wa nyota huyo, Kheri Chibakasa alisema kwa sasa wanasubiri kutafutwa na Yanga na kujua kama wataendelea naye au laa.
“Boban amebakiza miezi miwili ndani ya Yanga na mpaka sasa hakuna mazungumzo yoyote ambayo yamefanyika kati yetu hivyo tunawasubiri wao hata wapige simu kujua nini kinaendelea kwa ajili ya msimu ujao.
“Ofa zinaweza kuwepo sehemu nyingine lakini kwanza tunaipa nafasi Yanga kujua kama wataendelea naye au vipi japokuwa wachezaji wao karibu wote wa ndani ambao mikataba yao imemalizika hawajazungumza nao mpaka sasa,” alisema meneja.
Boban ni moja kati ya viungo bora wakongwe ambao waliwahi kutamba na klabu kama Simba, Coastal Union, Mbeya City, Friends Rangers na msimu uliopita na Yanga pamoja na timu ya Taifa, Taifa Stars.
The post Yanga Wamchunia Boban, Meneja Wake Afunguka appeared first on Global Publishers.
0 Comments