MAKOCHA wawili maarufu na wenye heshima kwenye soka la Tanzania, Jamhuri Kihwelu ‘Julio’ na Juma Pondamali wamekiri kwamba Yanga mpya itakuwa tishio. Julio na Pondamali wamejenga heshima ndani ya Simba na Yanga wakiwa kama wachezaji na makocha.
Julio ametamka kwamba katika Ligi ya msimu uliopita akiambiwa ni Kocha gani bora atamtaja Mwinyi Zahera wa Yanga kwani hajawahi kukosea tangu aanze kumjua na ndio maana anaamini kwamba Yanga mpya itatisha.
Amesisitiza kwamba Zahera ni Kocha mwenye jicho la kumsoma mchezaji na hata wachezaji wake wapya aliosajili watakuwa bora. Amesisitiza kwamba anampa heshima Zahera kutokana na mambo makubwa aliyofanya na Yanga mpaka kumaliza nafasi ya pili licha ya hali ngumu iliyokuwa kikosini pamoja na wachezaji kugoma mara kwa mara na misimamo yake.
“Nawapongeza sana Yanga kwa kuchagua viongozi wanaojua nini maana ya soka, kama walivyofanya kwa kumchagua Mwenyekiti wao Mshindo Msolla ambaye kwa levo yake ni kocha mkubwa aliyefundisha timu za taifa letu. Fredrick Mwakalebela pia ameongoza mpira kwa levo ya juu kabisa ya shirikisho letu.
“Kwa kufanya hivyo ninapata imani kubwa ya Yanga kufanya vema msimu ujao kwani ukichanganya uwezo wao na ule wa kocha wao Zahera utagundua namna gani walivyojipanga na ndiyo maana wamempatia Zahera jukumu lote la usajili,”alisema Julio ambaye ni mwanachama wa Simba.
“Zahera amefanya Skauti ya kutosha ni kocha mwenye jicho la kuona wachezaji wazuri na huwa hakosei, wachezaji wote ambao ameamua kuwasajili mapema, kocha hawezi kusajili harakaharaka hivyo atakuwa alishafanya skauti yake mapema kabisa.
“Hata yule beki (Lamine Moro) aliyefanya majaribio Simba na kuachwa yawezekana kabisa ni mzuri na akaja kuwashangaza Simba kwani walimuacha kimakosa maana mchezaji huwezi kumpima kwa muda mfupi kama ule.
“Hivyo uamuzi wa Zahera kusajili mapema ni mzuri sana kwani ameona mapungufu kwenye kikosi chake kwani wachezaji wetu wazawa ni wazuri lakini wana matatizo sana ya kutojitambua hivyo kwa kutazama hayo ninaimani kabisa wote aliyosajili ni majembe, hata kwa beki wake wa kulia Paulo Godfrey alivyompandisha na anavyoonyesha uzuri wake unaona kabisa Zahera ni Kocha,” alisema Julio.
Kwa upande wa Kocha wa Makipa wa Yanga Juma Pondamali alisema: “Yanga ijayo itatisha kwani kocha amefuata makubaliano ya benchi la ufundi kwa kusajili watu nane kama tulivyopanga.”
“Tulihitaji Kipa wa kigeni,Straika wawili wa kati na wawili wa pembeni, ila pia nafasi ya mabeki wawili wa kati na viungo wawili wa kati hata beki ya kushoto,”aliongeza Pondamali.
Habari za uhakika ambazo Spoti Xtra ilizipata jana ni kwamba Yanga ilimchomoa kwenye kambi ya Taifa Stars, kipa wa Mbao, Metacha Mnata na kwenda kumalizana nae fasta. Zahera anaamini kwamba Metacha ataleta changamoto kubwa kwenye safu yake ya ulinzi akiwa sambamba na Mkenya, Farouk Shikalo na Ramadhani Kabwili ambaye alikuwa na msimu mzuri.
USIPIME MAZOEZI YA TAIFA STARS Uwanja wa Taifa
The post Sasa Yanga Imeiva appeared first on Global Publishers.
0 Comments