

Mjadala mkali umezuka kwenye mitandao ya kijamii kufuatia maoni ya Rostam Aziz, Bilionea na Mwanachama wa Yanga ambaye amependekeza Yanga isifuate mfumo wa kumilikiwa na mtu mmoja au kutegemea wafadhili
Wengi wanaompinga Rostam wanaamini mpira wa sasa ni biashara, unahitaji uwekezaji mkubwa na jambo hilo halitawezekana kama watu wenye fedha hawataruhusiwa kuwekeza
Imetolewa mifano ya timu nyingi, kama ligi kuu ya Uingereza, Italia, Ufaransa na hata hapa Afrika mfumo wa uwekezaji wa watu wenye fedha ndio hutumiwa zaidi
Hata hivyo, mfumo aliopendekeza Rostam unaweza kuwa na mafanikio kama utaendeshwa vile inavyotakikana
Na ndio maana Rostam akaenda mbali kwa kusema yuko tayari kuwapeleka nje ya nchi viongozi wa Yanga wakajifunze uendeshaji huo au kuwaletea wataalam hapa hapa nchini
Timu kama Fc Barcelona, Real Madrid na Athletic Club za ligi kuu ya Hispania hazimilikiwi na tajiri mmoja na zimefanikiwa kupitia mifumo yao ya wanachama
Hata hizo timu zinazomilikiwa na matajiri haziufikii utajiri unaomilikiwa na timu kama Real Madrid na Fc Barcelona
Tatizo ninaloliona mimi wengi wanadhani kwa mfumo uliopendekezwa na Rostam, timu itategemea kujiendesha kwa fedha za wanachama pekee na watahitaji kuchanga kila mwaka jambo ambalo sio sahihi
Ninachofahamu mimi kila mwanachama wa klabu ni lazima alipie uanachama wake kwa mwaka.
Kinachofanyika ni kuweka madaraja ya Wanachama kulingana na uwezo wao kifedha ambapo wapo ambao uanachama wao utawagharimu zaidi ya wengine kulingana na daraja walilopo
Mwanachama wa daraja la juu anakuwa na faida 'flani' zaidi ya mwanachama aliye daraja la chini
Mfano Real Madrid na FC Barcelona zina kundi la wanachama wanaofahamika kama 'socios' ambao wanapewa mamlaka ya kuchagua viongozi wa timu
Mfumo huo unatoa wigo mpana kwa makampuni kujitokeza kuidhamini timu lakini pia timu itaendelea kuingiza mapato kupitia mauzo ya jezi na haki za matangazo ya televisheni
Ifahamike mfumo huu ni mahsusi kwa timu zenye wanachama wengi na sio kila timu inaweza kuufuata
Jambo la msingi ni Wanachama wa Yanga kupatiwa elimu ya kutosha kuhusu mfumo huu, kisha ni wao watakaoamua kama utawafaa au la



0 Comments