Windows

Makandarasi wavivu kunyimwa zabuni


Serikali imeziagiza halmashauri za wilaya, miji, majiji na manispaa zisitoe zabuni kwa makandarasi wavivu, wazembe na wasiowajibika ipasavyo na wenye tabia ya kuchelewesha maendeleo.

Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso ametoa agizo hilo juzi mjini Itigi wilayani Manyoni mkoani Singida baada ya kukagua ujenzi wa mradi wa maji katika vijiji vya Itigi, Majengo, Mlowa, Songambele, Tambukareli na Zinginali katika halmashauri hiyo.

Aweso alisema makandarasi wavivu siku zote wamekuwa changamoto kubwa kwenye miradi hiyo kufuatia kushindwa kutimiza majukumu yao kulingana na mikataba wanayowekeana na mamlaka husika; hivyo kuchelewesha huduma mbali mbali za kijamii kuwafikia wananchi wake kwa wakati muafaka.

"Serikali haiwezi kuendelea kuwabeba wakandarasi wasioheshimu masharti ya mikataba yao. Hivyo naagiza halmashauri zote nchini kuhakikisha zinakuwa makini katika kuchagua wakandarasi wachapa kazi tu na si vinginevyo,"alisisitiza Aweso.

"Alitoa kauli hiyo baada ya kuelezwa na Mhandisi wa Maji wa Halmashauri ya Itigi, Evaristo Mgaya kuwa mkandarasi anayejenga visima vitano vinavyotarajiwa kuhudumia vijiji sita, Nangai Engineering Co. Ltd alikuwa amefanya kazi hiyo kwa asilimia 35 tu huku ikiwa imebaki miezi miwili mkataba uishe.

Akionekana kukerwa na hali hiyo, akiwa eneo hilo la kazi, alimpigia simu Mkurugenzi wa kampuni hiyo na kumtaka aonane naye siku inayofuata mjini Itigi ili atoe maelezo ya kina juu ya utendaji kazi wake.

Ameonya wahandisi wa maji wasio waaminifu kujirekebisha mara moja vinginevyo ifikapo Julai mosi mwaka huu serikali itakapoanzisha rasmi Wakala wa Maji Vijijini, hawatakuwa watumishi wake.

"Tutakapoanzisha Wakala wa Maji Vijijini hatutakubali kuendelea na wahandisi wanaohujumu jitihada za serikali. Wenye changamoto tutawafikisha Bodi ya Wahandisi kujieleza na wale waliokithiri kwa vitendo vya rushwa, tutawakabidhi Takukuru ili washughulikiwe,"alifafanua Naibu Waziri Aweso.

Post a Comment

0 Comments