KAMA wewe ni kijana mwenye ndoto ya kuzamia Afrika basi habari ikufikie kuwa staa wa Hip Hop Bongo, Kala Jeremiah, ametinga leo ndani ya Global Group, Sinza-Mori jijini Dar na kuonyesha kuwa hapendezwi na mawazo hayo!
Kala ameweka sababu ya kutoa wimbo wake mpya wa Amerika kuwa Waafrika wengi hawathamini walipotoka na kuzamia nje ya nchi.
Akizungumza na +255 Global Radio kupitia kipindi cha Bongo 255 kinachosimamiwa na vichwa hatari viwili, Sechelela Mazanda na Stewart George, Kala alisema kuwa yeye ni mtu anayefuatilia kwa ukaribu habari nyingi za vijana nje ya nchi.
“Mimi ni mtu ambaye nafuatilia sana-sana habari za kimataifa. Naona vijana wengi wamekamatwa na kuhifadhiwa kwenye makontena, nawaza sana vijana kweli wanafanya hivi, hawaoni ombaomba huko nje ya nchi? Wale wanaopewa pa kulala na kula hawawaoni? Unakuwa kijana wa aina gani mpaka ukubali kuchukuliwa kama mtumwa?
“Mimi ni Mwafrika kweli kwenye mambo yanaoikumba Afrika, hata mtoto wangu anaitwa Alama kwa sababu ya uafrika wangu, mimi ni Mwafrika ambaye nipo ‘deep’ nikiona jambo linatokea Afrika naona bado Afrika tunakubali kutawaliwa kwa hiyo ndiyo sababu ya kuachia Wimbo wa Amerika ambao una ujumbe unaoenda na wakati ili kila kijana wa Kiafrika ajue,” alisema Kala.
Kala pia aliongelea video hiyo ya Amerika ambayo wanaonekana vijana kama machizi na wengine wa kawaida wakiingia na kutoka.
“Ni stori kama ya kweli kuna mtu alishaendaga lakini hakukuwa na utaratibu wowote ikabidi familia iuze shamba au ng’ombe ifuate mwili wa mpendwa wao, mambo ambayo yanatokea sana kwa hiyo ni kama mama ameuza shamba afuate mwili wa mtoto wake Ulaya.
“Pale kwenye video unaona machizi kama watatu wanazuiwa kuingia ndani, hawana pasipoti wakaamua kutengeneza bendi na kuimba lakini nyuma yake kuna watu wanakwenda Marekani na kurudi wasafi. Kwa wale machizi wanawakilisha machizi wengi sana wanaotaka kutoboa bila mpango maalum,” alimaliza kuongea Kala.
Ili kusikiliza Global Radio ni rahisi sana! Ingia kwenye Playstore katika simu yako ya mkononi kisha tafuta +255 Global Radio na baada ya hapo utapata kusikiliza vipindi vyote vya kijanja.
The post Hii ndiyo sababu ya Kala kuimba Amerika appeared first on Global Publishers.
0 Comments