Windows

Fursa nyingine ya Simba kutikisa Afrika



KATI ya timu 20 zilizoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita wa 2018/19, hakuna ubishi kuwa Simba ndiyo ilikuwa na kikosi bora zaidi.

Simba walionesha ubora huo uwanjani na waliweza kucheza mechi nyingi kwa ushindani wa hali ya juu kutokana na upana wa kikosi chao.

Ilidhihirika wazi hasa walipoweza kutetea taji lao la Ligi Kuu Bara na pia, kuweka rekodi ya kutinga hatua ya robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika.

Katika michuano hiyo ya kimataifa, Wekundu wa Msimbazi hao walitembea na mkakati mmoja tu ambao ni kutumia vizuri uwanja wa nyumbani.

Walifanya hivyo kuanzia hatua ya awali hadi walipovuka lengo lao na kufika robo fainali.

Katika mechi za nyumbani, Simba ilicheza soka la ubora unaoridhisha dhidi ya wababe wa Afrika kama vile TP Mazembe na AS Vita zote za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Kama hiyo haitoshi Simba iliyobebwa na sapoti ya mashabiki wake, iliweza kuwatambia mabingwa wa kihistoria Afrika, Al Ahly ya Misri na hata wakali wa Algeria, JS Saoura.

Kutinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa, ndiyo hasa kilichoifanya Simba kuwa gumzo Barani Afrika kwa sababu ni timu ya kwanza kufanya hivyo katika historia ya soka la Tanzania.

Katika kuhitimisha msimu wao wa mafanikio, Wanamsimbazi hao walipata zali la kucheza na wakali wa Hispania, timu ya Sevilla inayoshiriki Ligi Kuu ya nchi hiyo maarufu kama La Liga.

Pamoja na kufungwa mabao 5-4 na Sevilla kwenye mechi iliyochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, lakini soka walilolionyesha lilitosha kuithibitishia Dunia kuwa Simba si timu ya mchezo mchezo.

Wakati wapenzi wa soka hapa nchini na kwingineko wakidhani kuwa Simba imemaliza kazi, kuna fursa nyingine imejitokeza kwa klabu hiyo kuzidi kujitangaza Afrika.

Fursa hiyo si nyingine, bali ni kupitia michuano ya Kombe la Mataifa Afrika (Afcon 2019), inayotarajiwa kufanyika nchini Misri baadaye mwezi huu.

Katika michuano hiyo inayotarajia kuanza Juni 21 hadi Julai 19, mwaka huu, Simba itakuwa na wachezaji tisa wanaotarajia kuonekana nchini Misri wakiwa na timu zao za Taifa.

Emmanuel Okwi

Ni straika aliyefanya makubwa msimu uliopita akiwa na Simba, licha ya kwamba anatarajia kuondoka katika kikosi hicho, lakini atakuwepo na timu yake ya Uganda huku akiiwakilisha Simba.

Okwi ambaye ameifungia Simba mabao 15 msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara, ataipeperusha bendera ya Uganda ‘The Cranes’, tena akiwa ni miongoni mwa wachezaji wa kikosi cha kwanza.

Jjuuko Murshid

Beki wa Simba atakayeonekana Afcon akiwa na kikosi cha The Cranes, japo msimu uliopita hakuonekana uwanjani mara kwa mara kutokana na uwepo wa Pascal Wawa.

Pamoja na hilo, Murshid ni mmoja wa nyota ambao Simba watajivunia uwepo wake nchini Misri.

Aishi Manula

Mlinda mlango huyo bora wa Simba kwa mwaka wa pili mfululizo naye ataiwakilisha klabu yake hiyo, lakini akiwa na timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, ambayo inashiriki Afcon kwa mara pili.

Manula amekuwa kipa namba moja wa Taifa Stars kwa muda mrefu, kutokana na uwezo wake mkubwa awapo mbele ya milingoti mitatu, akitarajiwa kung’ara Misri.

Shomari Kapombe

Kikwazo kikubwa kwa Kapombe kimekua ni majeraha ya mara kwa mara ambayo yamemfanya kutoonekana na jezi ya Taifa Stars na Simba kwa muda mrefu.

Lakini kule Misri atakuwepo na timu ya kocha Emmanuel Amunike kwa maandalizi za Afcon baada ya afya yake kutengemaa, hivyo kutoa fursa kwake kudhihirisha ubora wake.

Francis Kahata

Ni sura mpya inayotarajiwa kuonekana katika kikosi cha Simba msimu ujao na pia kwenye michuano ya Afcon baadaye mwezi huu, akiwa na timu ya Taifa ya Kenya ‘Harambee Stars’.

Kahata ameelezwa kusaini mkataba wa awali na Wekundu wa Msimbazi hao baada ya kumalizana na Gor Mahia, hivyo iwapo dili hilo litakamilika, huenda winga huyo akaitangaza Simba huko Misri.

Jonas Mkude

Ni mmoja wa viungo wanaowavutia mashabiki wengi wa soka Tanzania, hasa wa Simba ambao hawataki kusikia habari ya kuondoka Msimbazi hata kidogo.

Mkude aliingia kwenye historia ya soka la Tanzania kwa kuchangia mafanikio ya kufuzu Afcon baada ya kipindi kirefu na ataiwakilisha Simba akiwa kwenye kikosi cha Taifa Stars.

Erasto Nyoni

Ubora wa beki huyo umemfanya awe kivutio kwa mashabiki na wachezaji wenzake wa Simba, hilo likidhihirishwa na hivi karibuni kuibuka beki bora wa tuzo za Mo Dewji.

Katika kuonyesha jinsi anavyokubalika ndani ya timu, Nyoni alichaguliwa na wachezaji wenzake kama mchezaji mcheshi na mwenye mvuto wa kipekee miongoni mwao.

Lakini pia, kiwango chake ndani ya Simba, kimemfanya awepo katika kikosi cha Taifa Stars kwa muda mrefu na anaingia katika rekodi ya kushiriki Afcon, mwaka huu.

John Bocco

Straika huyo mkali wa kuzifumania nyavu nchini tangu akiwa anaichezea klabu ya Azam, amekuwa hakosekani katika timu ya Taifa ambapo mwaka huu atakuwa na kikosi hicho akiwa ni mchezaji wa Simba, aliyefanya vizuri msimu uliopita kwa kufunga mabao 17.

Mohammed Hussein

Beki huyu wa kushoto maarufu kwa jina la Tshabalala, aliendeleza ubora wake msimu uliopita kwa kufanikiwa kumweka benchi beki Mghana, Asante Kwasi, kitendo kilichomvutia Amunike na kumjumuisha katika kikosi chake.

Je, nyota hao wa Simba wakiwa Misri watauwasha moto na kuipa mafanikio Taifa Stars? Hilo ni suala la kusubiri na kuona kama si kusikia.

Post a Comment

0 Comments