KOCHA Mwinyi Zahera hataki utani kabisa, baada ya kuhakikishwa na mabosi wake wa Jangwani kwamba mchezaji yeyote atakayemtaka basi atasajiliwa, naye fasta amechangamka baada ya jana Alhamisi kukwea pipa.
Kocha huyo amesafiri kwenda kwao DR Congo, lakini habari za ndani kutoka Yanga ni kwamba safari yake itamfikisha Benin ili kwenda kumalizana na straika mmoja matata wa nchini huyo, ila sio yule Marcelin Degnon Koupko aliyewahi kuja kutesti zali Jangwani.
Kwa wanaokumbuka Koupko anayeiochezea Buffles du Borgou FC ya Benin, alikuja nchini mwaka jana ili kusajiliwa, lakini alitakiwa kufanyiwa majaribio naye akagoma na kutibuana na Zahera.
Taarifa kutoka ndani ya Yanga zinasema Zahera ameenda Benin kufuata jembe jingine kabisa ambalo amekuwa akilifuatilia kupitia michuano ya mchujo ya kuwania fainali za Afcon 2019 ambapo Benin ilifuzu.
Hata hivyo, chanzo hicho kimeshindwa kutaja jina la mchezaji huyo wala klabu yake ila,kimesisitiza anakipiga Timu ya Taifa ya Benin ambayo imepangwa Kundi F sambamba na Cameroon, Ghana na Guinea Bissau.
“Kweli kocha kaondoka asubuhi (jana) , lakini safari yake inaenda kumfikisha Benin kuna mchezaji anataka kumalizana naye, kwa vile anatakiwa baada ya mechi ya Mbeya City kukutana na uongozi kuwapa bajeti na pendekezo la wachezaji anaowataka,” kilisema chanzo hicho.
Zahera aliwahi kunukuliwa na Mwanaspoti kuwa kuna majembe kama manane ya ndani na nje ya nchi ambayo anayataka katika kikosi chake, huku wageni wakitoka Benin, Guinea, Zimbabwe na DR Congo, bila kutaja majina ingawa ilikuja kubainika straika Mzimbabwe inayempigia hesabu ni Roderick Mutama aliyepo FC Lupopo ya DR Congo.
WANNE WATULIZWA
Huku nyuma kocha huyo amewatuliza mzuka wa nyota wake wanne ambao walikuwa na presha ya kutemwa baada kuwapa nafasi katika mechi hizi za mwisho ili kuwaongezea ulaji Jangwani.
Baada ya uongozi mpya wa Yanga chini ya Mwenyekiti Dk. Mshindo Msolla kumpa rungu la kusimamia usajili na mchezaji yeyote anayemtaka, Mkongoman huyo amechangamkia dili hilo.
Awali kulikuwa na tetesi Amissi Tambwe, Mateo Anthony, Haji Mwinyi, Juma Abdul, Pius Buswita, Said Juma ‘Makapu’, Thaban Kamusoko, Maka Edward, Buruhani Akilimali na kipa Ibrahim Hamid wamekalia kuti kavu.
Hata hivyo, wakati Ligi Kuu ikielekea ukingoni, upepo unaonekana kugeuka na kuanza kuwaendea vizuri nyota wanne kati ya wale waliokalia kuti kavu ambao wameonekana kuanza kufanikiwa kumshawishi Zahera kupendekeza waongezewe mikataba.
Nyota hao waliokuwa miongoni mwa wasiopewa nafasi na Zahera katika idadi kubwa ya mechi msimu huu, wameonekana kubadilika ghafla na kumfanya kocha huyo awape nafasi ya kutosha katika mechi za mwishoni jambo linalotoa ishara kuwa huenda wakaondoka kwenye mkumbo wa kutemwa.
Mabeki Mwinyi na Abdul na viungo Makapu na Kamusoko wamekuwa wakitumiwa mara kwa mara kwenye mechi za mwishoni za ligi tofauti na ilivyokuwa mwanzoni.
Mwinyi anayecheza nafasi ya beki wa kushoto licha ya kuonekana kushindwa kufua dafu mbele ya Gadiel Michael, ametumia vyema kuumia kwa mwenzake kumshawishi Zahera kumpa nafasi katika dakika za jioni.
Juma Abdul, sasa hivi anapangwa mara kwa mara huku Zahera akimsogeza juu, Paul Godfrey ‘Boxer’ ambaye sasa anapangwa kama winga wa kulia.
Lakini pia Zahera amekuwa akiwatumia viungo Makapu na Kamusoko ambao nao walikuwa hawapewi nafasi kwenye kikosi cha kwanza kutokana na uwepo wa Feisal Salum, Papy Tshishimbi, Mohammed Issah ‘Banka’ na Haruna Moshi ‘Boban’ lakini katika mechi za mwishoni kocha huyo amekuwa akiwapa sana nafasi.
Haijulikani kama ni mtego ambao kocha huyo ameamua kuwatega wachezaji hao wanne ili wajihukumu kabla hajafanya maamuzi au amebadili maamuzi na kuwaweka kwenye mipango yake kwa ajili ya msimu ujao lakini mwenyewe Zahera amedai anafanya hivyo kutokana na kuridhishwa na viwango vyao kwa sasa.
“Unajua mpira wa Tanzania nimeona ni wa ajabu, mashabiki na hata wanachama wanataka kuwa makocha wa mpira kwa kunipangia kikosi, hili sio sawa kabisa kwangu mimi ni muumini mkubwa wa mazoezi hivyo mtu akifanya vizuri mazoezini ndio anajihakikishia namba kwenye kikosi changu,” alisema Zahera.
Wakati mambo yakiwanyookea wanne hao, hali bado ni tete kwa kina Akilimali, Buswita, Hamid, Mateo, Tambwe na Maka Edward ambao bado wamekuwa hawapati nafasi kikosini
0 Comments