Baada ya kuivua Gor Mahia ubingwa SportPesa Super Cup, Mbao FC ndio timu gumzo zaidi katika michuano hiyo.
Mbao FC kutoka Mwanza, imemaliza ubabe wa miaka miwili mfululizo wa Gor ambayo ilibeba kombe hilo mara mbili mfululizo.
Gor ilikuwa mbabe hata kwa Simba, lakini ikakutana na Mbao za Mwanza ilizoshindw a kuzibeba.
Kikosi cha Mbao FC sasa kinacheza nusu fainali dhidi ya Kariobangi Sharks ya Kenya pia, kesho.
Mbao inayoshika nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara jana Jumatano ilifanya maajabu kwa kuwaondosha Gor Mahia ya Kenya ambao ni mabingwa watetezi wa michuano ya SportPesa Super Cup.
Timu hizo zilimaliza dakika 90 zikiwa sare ya bao 1-1 yaliyofungwa na Denis Oliech wa Gor Mahia dakika ya 52 na Aboubakary Ngalema wa Mbao dakika ya 76.
Zilipokwenda kwenye penalti Mbao ilishinda 4-3 na kuwaacha Wakenya hao wenye mastaa kama Francis Kahata, Jacques Tuyisenge wakiwa hawana la kufanya.
Kocha wa Mbao, Ally Bushiri alisema; “Kwanza tuliwaheshimu sana Gor Mahia, tukaamua kukaa na mpira muda mwingi, lakini vilevile kipigo cha Yanga cha jana (juzi) kilitufanya tuongeze umakini ili kutunza heshima ya nchi.”
Kwa matokeo hayo, Mbao anakwenda kucheza nusu fainali na Kariobangi Sharks kesho Ijumaa saa 10:15 jioni.
.
0 Comments