Saa 24 zijazo, Simba inaweza kutangazwa bingwa tena kesho Jumanne kama ikipata ushindi ama hata sare dhidi ya Singida United kwenye Uwanja wa Namfua.
Kagere aliyesajiliwa na Simba msimu huu akitokea Gor Mahia, jana alifunga mabao mawili na kuipa timu yake ushindi muhimu mbele ya Ndanda FC, lakini pia aliandika rekodi ya mabao Msimbazi akivunja rekodi ya Emmanuel Okwi ya msimu uliopita.
Mnyarwanda huyo pia alivunja rekodi iliyodumu miaka mitatu ya Amissi Tambwe wa Yanga aliyekuwa nyota wa kigeni aliyefunga mabao mengi katika msimu mmoja pale alipofunga mabao 21 katika Ligi Kuu msimu wa 2015-2016. Kagere amefikisha mabao 22 msimu huu akizidi kukinyemelea Kiatu cha Dhahabu kilichokuwa kinashikiliwa na Okwi aliyetwaa msimu uliopita na mabao yake 20.
Katika mchezo wa jana Simba ilishuka uwanjani ikisaka ushindi ili kumaliza udhia wa kubanana na watani zao Yanga ambao keshokutwa Jumatano wataikaribisha Mbeya City katika mfululizo wa ligi hiyo itakayomalizika Mei 28.
Ikicheza bila ya Okwi anayetumikia adhabu ya kadi tatu za njano, Kagere alithibitisha kuwa ni usajili bora kabisa kuwahi kufanya na Simba pale alipofunga mabao mawili ndani ya dakika tano na kuipa timu yake ushindi wa 28 msimu huu.
Ushindi huo umefanya Simba kufikisha pointi 88 baada ya mechi 35 na ikisaliwa na mechi tatu ambapo sare yoyote au ushindi dhidi ya Singida United kesho Jumanne itawafanya watangaze ubingwa mapema kabla ya kumalizika kwa msimu huu.
Yanga ina alama 83 baada ya mechi 36 ambapo itashuka uwanjani Jumatano na kama italazimishwa sare na Wagonga Nyundo hao, hata kama Simba itapoteza kesho basi itanyakua ubingwa kwani Yanga haitazikifia pointi ilizonazo Simba kwa sasa na mabao 74 iliyonayo.
Kagere alifunga bao la kwanza dakika ya 6 kwa shuti kali la mguu wa kushoto akimalizia
pasi ya nahodha John Bocco, kabla ya kurudi tena nyavuni dakika ya 11 akipenyezewa pasi na Clatous Chama na kuubetua mpira mbele ya kipa wa Ndanda Diey Makonga.
Mabao hayo yamemfanya Kagere kufikisha mabao 22 na kusaliwa na manne tu kuifikia rekodi iliyowahi kuwekwa na Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ aliyekuwa Yanga ya kufunga mabao 26 katika msimu mmoja akifanya hivyo mwaka 1998.
Pia, mabao hayo yamemfanya straika huyo kufikisha jumla ya mabao 36 katika mashindano yote tangu atue Msimbazi. Straika huyo amefunga mabao manne ya Kombe la Kagame, sita ya Ligi ya Mabingwa Afrika, mawili ya Kombe la Mapinduzi 2019, moja la Ngao ya Jamii na jingine la mechi ya kirafiki nchini Uturuki.
Ikumbukwe kuwa wanaomfuatia Kagere kwenye chati ya ufungaji bora ni Heritier Makambo wa Yanga na Salim Aiyee wa Mwadui wenye mabao 16 kila mmoja.
Kiujumla kipindi cha kwanza kilitawaliwa na Simba ambao kama washambuliaji wake wangekuwa makini basi wangepata ushindi mnono zaidi, na hata kipindi cha pili bado waliwabana Ndanda ambao walijitutumua kutaka kusawazisha mabao bila mafanikio.
Kwa dakika zote 90, Simba ilimiliki mpira kwa asilimia 70 dhidi ya 30 za wageni wao na ikipiga mashuti 16, sita yakilenga lango na mengine 10 yakitoka nje, huku wageni wakipiga sita tu yaliyopotea maboya.
katika mchezo huo Simba ilipiga kona 5 huku Ndanda ikitoka kapa, huku ikicheza faulo 13 dhidi ya 19 za Ndanda na kuotea mata tatu, huku Wana Kuchele wakiwa hawajaotea hata mara moja zaidi ya kuambulia kadi mbili za njano.
Mara baada ya mchezo huo, Kagere alisema amekuwa akifunga kwa sababu ya kujituma kwake na ushirikiano na wachezaji na hafanyi hivyo kwa kutaka kuchuana na mtu ila ni kwa vile hiyo ndio kazi yake.
0 Comments