Windows

Huyu hapa Mzee wa Penalti aliyempindua Samatta Ubelgiji

UKISIKIA mambo ni moto, mambo ni fire, ni katika mazingira kama haya. Kuna Mtunisia huyo, anaitwa Hamdi Harbaoui unayeweza kumwita ‘Mzee wa Penalti’, Kizungu zaidi ni Mr Penalty. Huyo bwana achana naye, anacheza ligi moja na Mbwana Samatta.
Hamdi (34) anayeichezea S.V. Zulte Waregem katika michezo ya Ligi Ndogo ‘Play Off’, mwishoni mwa msimu alitibua mambo kwa Samatta kwenye kinyang’anyiro cha kuwania kiatu cha dhahabu cha Mfungaji Bora.
Ukiangalia orodha ya mastaa waliokuwa wanawania kiatu cha dhahabu Ligi Kuu Ubelgiji ‘Jupiler Pro’ kabla ya michezo ya jana ya kufunga pazia la msimu, utabaini kuwa Mr Penalti alifanya yake wiki chache nyuma.
Tuanzie huku, baada ya kumalizika kwa mizunguko yote ya Ligi Kuu Ubelgiji kwa maana ya kila timu kucheza michezo 30, ligi yao huingia kwenye sura nyingine ambapo timu hugawanywa kwenye makundi tofauti kutokana na nafasi zilizoshika na kucheza Ligi Ndogo ‘Play Offs’.
Ligi Ndogo huchezwa ili kupata bingwa wa Juliper Pro, timu za kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya, Europa Ligi pamoja na kujinasua kutoshuka daraja.
Pia ligi hizo ndogo zimegawanywa kwenye namna mbili, Ligi ya Kwanza ni kwa timu ambazo zilimaliza kuanzia nafasi ya kwanza hadi ya sita ‘top six’ hizo hucheza ligi yao ndiyo walipokuwa kina Samatta na KRC Genk yake ambako walikomaa na mwishowe kutwaa ubingwa wiki iliyopita na jana kukabidhiwa rasmi taji lao.
JTimu zile zilizoshika nafasi ya saba na kuendelea hucheza Ligi Ndogo nyingine ambayo hugawanywa kwenye makundi A na B na huku ndiko lilikokuwa chama la Mr Penalti.
Sasa wakiwa kwenye sura tofauti za kuzipigania timu zao, Samatta akiwa kwenye Ligi Ndogo ya kwanza ambayo hutafuta bingwa na Mr Penalti kwenye kupigania nafasi ya kwenda Europa Ligi huko ndiko yalikotokea mengine.
Hamdi alitupia mabao saba kwenye Ligi Ndogo yao ya pili ya kutafuta timu za kucheza Ligi ya Europa na hivyo kumpita Samatta katika mbio za kuwania kiatu cha dhahabu kwa kufikisha mabao 25. Lakini unajua kwanini nimeamua kumpa jina la Mr Penalti? Ni kwa sababu mabao sita kati ya hayo saba ya mwisho amefunga kwa mikwaju ya penalti.
Hatanii kabisa Hamdi pindi anapoutenga mpira kwa ajili ya kupiga penalti kwa sababu katika mabao yake ya jumla 25 aliyofunga kwenye Jupiler Pro msimu huu, mabao 11 ameyafunga kwa matuta, aiseeh!! Huyo ndo’ Mr Penalti kama ulikuwa humfahamu.
Msimu huu wa 2018/19, Mr Penalti hakuna kipa ambaye ameamuacha salama pindi alipokuwa akipiga mikwaju yake ya penalti.
Samatta mwenye penalti moja tu ambayo aliifunga kwenye mabao 23 aliyofunga msimu huu kabla ya mchezo wa jana dhidi ya Standard Liege, siyo chaguo la kwanza kwenye upigaji matuta katika klabu yake ya Genk.

Post a Comment

0 Comments