Windows

Samatta aibua siri ya mabao 23 mpaka sasa

Genk. KATIKA apartment yake ya kifahari anayoishi katikati ya Jiji la Genk, Residente Albert, Samatta anafungua moyo wake kuhusu kilichomfanya afunge mabao mengi msimu huu.
Mpaka kufikia jana Jumapili kabla ya pambano la mwisho dhidi ya Standard Liege nyumbani Lumunus Arena tayari alikuwa amefunga mabao 23. Bao lake la 23 alilifunga mbele ya macho yangu katika pambano dhidi ya Antwerp.
Lilikuwa bao la pili la mechi baada ya kumtungua kipa wa kimataifa wa Uturuki, Sinan Bolat kwa shuti kali akiwa nje ya boksi na hivyo kuiweka Genk katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa.
“Tayari nimewajulia Wazungu” anasema Samatta akiwa anajiweka vema katika kochi la sebule yake. “Ni kitu cha kawaida unapokuja mgeni unahitaji kuzoea kwanza mazingira halafu baadaye unawasha moto. Ndicho kinachotokea,” aliongeza Samatta. Samatta mara nyingi amekuwa akituma picha mitandaoni akionekana akifanya mazoezi yake binafsi katika eneo moja lenye mchanga mwingi. Anakiri mazoezi binafsi yamemsaidia kwa kiasi kikubwa kufanya vema zaidi msimu huu.
“Unajua kocha anakuwa na mazoezi yake. Baada ya hapo kila mtu anakwenda kwake. Mimi nilihitaji kufanya mazoezi ya ziada kwa ajili ya kuwa fiti zaidi. Niliachana na utaratibu wa kawaida wa mazoezi na kuanza kujifua zaidi. Kila nilipojifua kwa mazoezi binafsi nilijiona mwepesi zaidi,” anakiri Samatta.
Anakubali kwa sasa amekuwa akifunga mabao ya kuibia zaidi tofauti na ilivyokuwa zamani kwa sababu kocha wake, Philippe Clement amekuwa akimtaka asimame katikati zaidi na asiende pembeni tofauti na staili yake ya soka iliyozoeleka.
“Kocha anataka nisimame pale mbele kama mshambuliaji wa kati. Zamani nilikuwa napenda kutokea pembeni lakini kwa sasa nasimama pale na kazi yangu ni kufunga tu. Kocha anatambua uwezo wangu wote wa kucheza katika staili tofauti lakini anataka nisimame mbele zaidi na nisihangaike sana.”
Hata hivyo, Samatta anawapa usia wachezaji mbalimbali nchini waitambue miili yao vema kabla ya kufanya mazoezi kwa nguvu. Sio kila mchezaji inabidi afanye mazoezi mazito.
“Inabidi ufanya mazoezi ya ziada kutokana na jinsi mwili wako ulivyo. Unawaona Ronaldo na Messi? Messi hafanyi sana mazoezi ili awe fiti lakini Ronaldo analazimika kufanya mazoezi kwa ajili ya kuwa fiti zaidi,” aliongeza Samatta.
Anakiri tofauti na msimu wa kwanza, msimu huu wa tatu anacheza na mastaa wanaocheza kitimu zaidi. Miongoni mwao ni Leandro Trossard ambaye ni mzaliwa wa hapohapo Genk pamoja na kiungo wa kimataifa wa Ukraine, Ruslan Malinovskyi.
“Wakati ule wa kina Leon Bailey huduma zilikuwa hafifu lakini sasa hivi tunacheza kitimu zaidi ndio maana nafunga zaidi na wenzengu pia wanafunga zaidi.”
Napata nafasi ya kumuhoji zaidi Samatta kuhusu chakula ambacho anakula. Nimemuuliza swali hili wakati tukiendelea kula ugali, dagaa na nguru, vyakula ambavyo aliagiza kutoka Tanzania. Jibu analonipa linaniacha hoi zaidi.
“Chochote unachotaka unakula lakini kivumbi unakutana nacho mazoezini. Wazungu wanataka matokeo tu hawataki blah blah. Siku moja kabla ya mechi unalala nyumbani lakini wanachotaka wao ni matokeo,” anasema Samatta.
“Huwa tunapewa ushauri wa vyakula vya kula lakini huwa hatusimamiwi na mtu. Unakuwa uko peke yako nyumbani kwahiyo unaweza kula chakula chochote unachojisikia lakini wenzetu huwa wanataka uwe fiti uwanjani. Wachezaji wenyewe wanajua chakula gani wale na chakula gani wasile lakini kama nilivyosema hausimamiwi na mtu,” anasema Samatta.
“Wakati mwingine naamini wachezaji wa nyumbani huwa wanapewa maandalizi mazuri zaidi ya mechi lakini hawajitambui. Yaani wanawekwa kambini na wanapangiwa vyakula vya kula. Wanapangiwa muda wa kulala na kuamka. Sisi huku ni tofauti lakini kila mtu anatambua wajibu wake na anapiga kazi. Ndio maana ya mwanasoka wa kulipwa,” anaongeza Samatta.
Kesho yake tunakuwa na ratiba ya kwenda kufanya mahojiano zaidi katika uwanja wao wa Luminus ambao wanachezea mechi zao za nyumbani. Ananipitia katika Hoteli ya Atlantis ambayo huwa nafikia nikienda Genk. Ananipitia na usafiri wa kifahari. Gari lake aina ya Range Rover. Gari la kisasa. Gari amenunua katika siku za karibuni na mara nyingi amekuwa akiposti mitandaoni akiwa na gari hii ya kisasa. Napata fursa ya kudodosa kiasi cha pesa alichotumia kununua gari hilo la kifahari. Midomo yangu inabakia wazi.
Je, amenunua gari kwa kiasi gani cha pesa za Kitanzania? Je, unafahamu kwanini ameamua kujenga msikiti Vikindu? Endelea kufuatilia kesho makala haya ya kusisimua kuhusu maisha ya ustaa ya nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania, Mbwana Samatta katika klabu ya Genk ya Ubelgiji.

Post a Comment

0 Comments