MWENYEKITI wa Klabu ya Yanga, Mshindo Msolla yuko kwenye mchakato wa kusaka kocha msaidizi mwenye vigezo ili aweze kumsaidia Mwinyi Zahera ili kuleta timu yenye ushindani msimu ujao.
Yanga inahitaji kufanya maboresho makubwa katika kikosi chake kwa ajili ya msimu ujao wa ligi kuu ambapo imejipanga kuboresha benchi la ufundi ili kuwa na ushindani zaidi.
Akizungumza nasi , Msolla amesema kuwa, wanachohitaji ni kuona wanakuwa na kikosi bora msimu ujao kwa kupata kocha msaidizi mwenye vigezo kupitia ‘wasifu’ CV watakazozipata na kudai kuwa wanaangalia zaidi kocha mzawa aweze kusaidiana na Zahera.
“Benchi la ufundi linahitaji kuwa na kocha msaidizi mwenye kiwango kizuri ili kuongeza nguvu ndani ya kikosi chetu, tutaangalia zaidi kocha mzawa ili aweze kuwa sambamba na kocha Zahera kufanya kazi.
“Katika nchi za wenzetu zilizoendelea kocha mkuu amekuwa akimtumia zaidi kocha msaidizi kwa kumtuma kwa ajili ya kwenda kufuatilia wachezaji wanaowahitaji kwa ajili ya kuwasajili hata ikiwa nje ya nchi ambaye anafuatilia mechi na mazoezi anayofanya mchezaji, hivyo tunahitaji msaidizi mwenye weredi atakayeshirikiana vyema na kocha mambo mbalimbali.
“Tukiachana na kazi ya kutafuta kocha, pia tutawatumia wachezaji wa zamani waliowahi kuichezea Yanga kuweza kuwatuma mikoani kwa ajili ya kusaka vipaji,” alisema Msolla.
0 Comments