Windows

Jeuri ya pesa Yanga yawang’oa Mkude,Chama,Manula




KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, uongozi mpya wa klabu ya Yanga, umeweka wazi dhamira yake ya kusajili wachezaji tegemeo waliomo ndani ya kikosi cha mahasimu wao, Simba.

Wachezaji ambao Yanga wanasema wameanza kufanya nao mazungumzo na wameshaonyesha dalili za kukubali kutua kwa Wanajangwani hao ni kipa namba moja, Aishi Manula, Jonas Mkude pamoja na Clatous Chama.


Aliyelithibitishia DIMBA ukweli wa taarifa hizo ni Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela, ambaye kwa kujiamini alisema wachezaji hao watatu wa Simba wanaweza kuonekana wakivaa jezi za Wanajangwani hao msimu ujao.

“Jonas Mkude tunajua kwamba anataka kwenda nje kucheza soka la kulipwa, hataki tena kuongeza mkataba Simba, lakini sisi tunataka kumbakiza, Manula (Aishi) naye mkataba wake umefikia ukingoni na tumeanza naye mazungumzo, japo Simba nao wamefanya naye mazungumzo lakini hawajafikia mwafaka kwa sababu anataka wampe milioni 150, Simba wamegoma.

“Kwa upande wa Chama tunajua ana mkataba, lakini tukikubaliana tunawafuata Simba na kuvunja mkataba kwa sababu tunamhitaji na tuna amini tutalimaliza vizuri,” alisema Mwakalebela.

Kiongozi huyo ambaye aliwahi kuwa Katibu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), alisema kuwa usajili ujao wa Yanga utakuwa si wa mchezo na mashabiki wasubiri kusikia na kuona kishindo kitakachovunja rekodi.

Alisema kwa namna hali ilivyo Yanga, hakuna kitakachoshindikana, pia akiwataka mashabiki wao kutulia akiwaahidi mambo mazuri yanayokuja mbele ya safari.

Yanga wanaweza kuwapata kirahisi Mkude pamoja na Manula kwani mikataba yao inafikia ukingoni, lakini ikionekana kuwa ngumu kwa Chama kwani mkataba wake bado unasoma Simba.

Inasemekana Mkude anataka kuondoka Simba na kwenda kutafuta maisha nje ya nchi na Yanga wameamua kuivunja safari hiyo na kuhakikisha anaungana na rafiki yake wa muda mrefu, Ibrahim Ajib, ambaye ni nahodha wa Wanajangwani hao.

Hii si mara ya kwanza kwa Mkude kuhusishwa na Yanga kwani enzi za uongozi wa aliyekuwa mwenyekiti wa timu hiyo, Yusuph Manji, inasemekana alitengewa milioni 80 akazitolea nje kutokana na mapenzi aliyokuwa nayo na klabu hiyo lakini msimu huu anaweza akachukua maamuzi magumu.

Taarifa hizo bila shaka zinaweza kuwachefua sana mashabiki wa Simba kwani wachezaji wote watatu waliotajwa kuanza mazungumzo na Yanga, ni wa kikosi cha kwanza.

Kwa upande wao Yanga ni kicheko tu kwani kocha wao mkuu, Mwinyi Zahera, alishasema anataka msimu unaokuja kusajili wachezaji watakaorudisha heshima ya timu hiyo na kutangaza ubingwa mapema ligi ikiwa bado mbichi.

Hata hivyo, dalili zinaonyesha kwamba sakata la usajili katika klabu hizo kongwe linaweza kuwa na mvutano wa hali ya juu kutokana na matumaini aliyotoa mwekezaji wa Simba, Mohamed Dewji ‘Mo’, kwa wachezaji wake alipowatembelea juzi.

Mo aliwataka wachezaji wote kutulia na kusubiri matunda ya kazi yao endapo watafanikiwa kutwaa ubingwa msimu huu, kazi ambayo ina asilimia kubwa kwa kikosi cha Simba.

source : Dimba

Post a Comment

0 Comments