Lakini kumbe mabosi wa klabu hiyo wanajua kila kitu kinachoendelea na kuanza mipango ya mapema ya kuhakikisha msimu ujao wanarudi kivingine katika Ligi Kuu Bara na michuano mingine yote watakayoshiriki na kuwapigia hesabu nyota kadhaa wa Simba.
Mabosi wa Yanga wameanza kumnyemelea Jonas Mkude na nyota wengine kadhaa wa Msimbazi, lakini vigogo wa Simba nao wameamua kula sahani moja kuhakikisha hakuna kifaa hata kimoja kinachomoka ndani ya kikosi chao.
Ishu ipo hivi. Baada ya Yanga kusikia Mkude na baadhi ya nyota wengine wa Simba wanaomaliza mikataba wamegoma kusaini mikataba wakitaka kuongezwa dau na lile walilopewa katika mikataba yao ya sasa fasta wakawapigia simu ili kuzungumza nao.
Mmoja ya waliovutiwa waya ni Mkude ambaye inaelezwa amekataa kupewa Sh 40 milioni za usajili kutoka Sh70 milioni alizosaini matika mkataba wake unaomalizika, lakini ghafla mabosi wa Simba nao wakaamua kumkalisha chini kijana wao na kumtaka abaki.
Habari kutoka kwa kiongozi wa juu wa Yanga aliyeingia madarakani hivi karibuni, alilidokeza Mwanaspoti akili yao ni kuwanyakua Mkude na kipa Aishi Manula ili kuziba nafasi ya Beno Kakolanya waliyeachana naye.
Kiongozi huyo aliyekataa kutajwa jina gazetini, alisema mchakato wa kukusanya fedha ndio unaowapa jeuri ya kuipora Simba majembe yao yaliyoifikisha robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na wakielekea kutetea taji lao la Ligi Kuu Bara.
“Hao wawili hatuna shida nao maana tumeshaongea nao na kuelewana kabisa ila jukumu tumeawaachia wenyewe kama wapo tayari kusaini Yanga pesa zinawasubiri mezani, ila kama hawatakuwa tayari kujiunga nasi basi tutatafuta vifaa vingine,” alisema.
Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela alipoulizwa juu ya taarifa hizo alisema ni kweli wachezaji hao wa Simba wanaweza kuvaa jezi za Yanga msimu ujao kwani wameshaanza kuzungumza nao, akiwamo Meddie Kegere.
“Mkude tunajua anataka kwenda nje kucheza soka la kulipwa, hataki tena kuongeza mkataba Simba, ila sisi tunataka kumbakiza, Manula naye mkataba wake umefikia ukingoni na tuna taarifa kuna dau anataka apewe Simba na wenzetu wamekwama, tumemuita na kumuahidi tutampa na Kagere pia kaingia katika rada zetu ingawa bado ana mkataba wa timu yake,” alisema Mwakalebela.
Hata hivyo, mabosi wa Simba baada ya kusikia tetesi hizo za kutaka kuporwa nyota wake hao wamedaiwa kufanya kila njia kuwakabisha, wakianza na wale waliokuwa wakitajwa kutakiwa na Azam FC kama John Bocco, Shomari Kapombe na Erasto Nyoni.
“Saizi ni kipindi cha usajili mtasikia mengi ni kweli nyota hao tumesikia walikuwa wanahusishwa na Yanga, ila nakuhakikishia hakuna nyota hata mmoja ataruhusiwa kuondoka Simba na kwenda Yanga au Azam, tumetenga kitita cha fedha kuwabakisha wachezaji wetu wote wanaomaliza mikataba wanabaki na kuongeza vifaa vingine vipya,” alisema mmoja wa Wajumbe wa Bodi ya Simba aliyeomba kuhifadhiwa jina.
MSIKIE MKUDE
Mwanaspoti lilimtafuta Mkude kutaka kauli yake juu ya kuziingiza klabu hizo kongwe nchini ikiwa ni mara nyingine tena kwani hata usajili wake uliopita Msimbazi ulikuwa ukitajwa kutakiwa Jangwani enzi za Yusuf Manji.
Mkude, alisema mpaka sasa bado hajasaini kokote. “Kwa muda huu siwezi kueleza lolote kuhusu kama nitasaini Yanga au kuongea na uongozi wa timu hiyo, lakini vilevile hata kueleza lolote kuhusu kubaki Simba kwani akili yangu ipo kwa ajili ya mechi leo jioni (jana), dhidi ya Ndanda nafikiri baada ya hapo ndio nitakuwa na majibu ya kutosha,” alisema kiungo huyo.
0 Comments