

BAADA ya vuta nikuvute na subira ya muda mrefu, hatimaye leo Yanga wanatarajia kufanya uchaguzi na kupata viongozi wapya watakaoiongoza timu hiyo kwa miaka minne ijayo.
Kwa mujibu wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) chini ya mwenyeikiti wake, Ally Mchungahela na Kamati Maalumu ya Yanga ya kusimamia uchaguzi huo, jana Jumamosi ndio ilikuwa mwisho wa wagombea kufanya kampeni kabla ya leo kupigiwa kura na wanachama wa klabu hiyo.
Uchaguzi huo unalenga zaidi kuziba nafasi za Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na wajumbe. Wagombea wengi kuanzia ngazi ya juu wamekuwa wakinadi sera zao juu ya kuikomboa timu hiyo kiuchumi na kuipeleka kimataifa zaidi.
Kiuhalisia ni wazi Yanga ilionesha kuyumba kiuchumi mara baada ya kujiuzulu kwa Yusuf Manji aliyekuwa mwenyekiti wa Wanajwangani hao kabla ya baadaye Makamu Mwenyekiti, Clement Sanga naye kubwaga manyanga na kufuatiwa na wajumbe wengine wa Kamati Tendaji.
Lakini sasa wagombea wengi watakaojua hatma zao baada ya uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika katika Bwalo la Maofisa wa Polisi, Oysterbay Dar es Salaam wameonekana kuwa na mbinu tofauti za kuirejesha Yanga na kuwa tishio zaidi ya miaka iliyopita huko nyuma.
Suala la mabadiliko ya muundo wa uendeshaji wa kisasa wa klabu pia imekuwa ikitawala kwenye vinywa vya wagombea wengi ikionekana ni kati ya njia nadhifu itakayoivusha Yanga hapo ilipo na kuanza kukimbizana na timu vigogo wa Afrika.
Wanachama wataingia kwenye uchaguzi huo wakiwa na majina matatu ya wanaowania nafasi ya mwenyekiti baada ya Elius Mwanjala kujiondoa dakika za mwisho akidai ana majukumu mengi. Waliosalia ni Jonas Tiboroha, Dk Mshindo Msola na Baraka Igangula, ambaye jana alitangaza kujitoa.
Wakati katika nafasi ya makamu mwenyekiti wanaotoana jasho ni Janeth Mbena, Fredrick Mwakalebela, Salum Chota, Yono Kevela na Tito Osoro. Wajumbe wanaowania kuingia kwenye Kamati Tendaji ili kupata nafasi ya kuijenga upya timu hiyo inayoshikilia rekodi ya kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara 27 ni Ally Sultan, Benjamin Mwakasonda, Frank Kamugisha, Seko Kingo, Hamad Islam, Sharif Makosa, Leonard Marango, Bahati Mwaseba na Sylvestre Haule.
Wengine ni Saad Khimji, Rodger Gumbo, Nassor Matuzya, Abdallah Chikawe, Said Ntimizi, Palina Conrad, Elius Mkumbo, Suma Mwaitenda, Seif Hassan, Dominic Albinus, Cyprian Musiba na Haruna Batenga Uchaguzi huo unatarajia kuanza kuunguruma mapema saa 2:00 asubuhi huku Mchungahela akisisitiza kuwa wamejipanga vya kutosha kwa ajili ya kufanikisha zoezi hilo, akithibitisha kuwa hali ya usalama pia itakuwa juu katika muda wote wa zoezi hilo.



0 Comments