Windows

Yanga kumfanyia umafia Kagere



KIKOSI cha Yanga kimeendelea na mazoezi yake katika Uwanja wa Chuo cha Polisi, Dar es Salaam, huku kocha mkuu wa timu hiyo, Mwinyi Zahera, akisisitiza ushindi ni lazima kesho watakapowavaa Mbeya City.

Yanga ndio wenyeji wa mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaopigwa Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam, huku wakiweka mkakati kabambe wa kumtengenezea pasi za mabao mshambuliaji wao, Heritier Makambo, ili aweze kumpita Meddie Kagere wa Simba na hivyo kutwaa kiatu cha dhahabu cha ufungaji bora.

Hadi sasa, Kagere ndiye anayeongoza kwa ufungaji mabao, akiwa amecheka na nyavu mara 22, huku Makambo akiwa na mabao 16 kibindoni.

Ili Makambo aweze kumpita Kagere, atahitaji kufunga mabao zaidi ya manne katika kila mechi kati ya mbili zilizobaki ambapo baada ya kuvaana na Mbeya City, watapepetana na Azam kuhitimisha ligi hiyo.

Juu ya mchezo wao wa kesho, Zahera ameliambia BINGWA kuwa kikosi chake kipo katika hali nzuri hivyo kesho lazima washinde.

Alisema wanajitupa uwanjani wakiiheshimu Mbeya City kutokana na rekodi waliyonayo, japo hilo haliwapi shida, wakiamini pointi tatu kesho ni zao.

“Jana tumefanya mazoezi ya kujitoa uchovu leo yanaendelea lakini kikosi kipo vizuri tunaamini ushindi utapatikana,” alisema.

Kwa upande wake Meneja wa Yanga, Hafidhi Saleh, alisema watawakosa nyota wawili katika mchezo huo kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo majeruhi, huku akisisitiza mkakati wao wa kumwezesha Makambo kuibuka mfungaji bora.

Alisema watamkosa beki wao wa kati, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, anayetumikia adhabu ya kadi tatu za njano na Gadiel Michael ambaye bado anauguza majeraha.

“Tumefanya mazoezi kama kawaida Polisi na vijana wapo tayari kwa ajili ya mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu na mashabiki mbalimbali nchini.

Wakati Hafidh akiyasema hayo, Kocha wa Mbeya City, Ramadhani Nsanzurwimo, alisema Yanga wasitarajie mteremko katika mechi hiyo.

“Utakuwa mchezo mgumu ila hilo halinipi wasiwasi kwani morali kwa wachezaji wangu ipo juu, natarajia kupata matokeo kama ilivyokuwa kwenye mechi yetu iliyopita,” alisema.

Yanga inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa sasa baada ya kukusanya pointi 83 huku wapinzani wao wa jadi Simba wakiwa ndio vinara kwa pointi zao 88.

Post a Comment

0 Comments