Windows

AUSSEMS ‘BYE BYE’ SIMBA



KOCHA Mkuu wa Simba, Patrick Aussems, yupo mbioni kuachana na timu hiyo, huku uongozi wa Wekundu wa Msimbazi hao ukiwa umeanza mchakato wa kumsaka mbadala wake.

Habari za uhakika zilizolifikia BINGWA wikiendi iliyopita, zinasema kuwa kocha huyo amefikia uamuzi huo kutokana na kutoridhishwa na mshahara anaolipwa.

Imedaiwa kuwa kocha huyo raia wa Ubelgiji, analipwa kitita cha Dola za Marekani 10,000 (takribani Sh mil 22.9) kwa mwezi.

Hayo yanatokea wakati Aussems akiwa ameipa mafanikio makubwa Simba kwa kuifikisha robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku pia ikiwa na nafasi kubwa ya kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kocha huyo alitua Simba mwanzoni mwa msimu huu baada ya kutimuliwa kwa Mfaransa, Pierre Lichantre, aliyeipa timu hiyo ubingwa wa Bara msimu uliopita.

Juu ya habari hizo za kuondoka kwake Simba, BINGWA jana lilizungumza na Aussems aliyekiri hilo, japo aliweka wazi kuendelea kuwapo Msimbazi iwapo ataongezewa mshahara.

“Naweza kusema katika timu ambazo nimefanya kazi kwa amani, lakini kwa presha kubwa katika klabu za Afrika, ni Simba. Natamani kuendelea kuwepo, lakini kama uongozi utaniangalia tena kivingine, japokuwa ninaisaidia timu, lakini na mimi naangalia masilahi yangu,” alisema Aussems.

Mbelgiji huyo ambaye kibarua chake Simba kinafikia ukingoni mwezi ujao, alisema amepokea ofa nyingi hasa baada ya kuifikisha timu hiyo robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini bado hajakubaliana na klabu yoyote akisubiria kauli ya mabosi wake wa sasa kama bado wanamhitaji.

Hata hivyo, Aussems alisema kuwa inahitaji uvumilivu wa hali ya juu kufundisha timu za Afrika kwani asilimia kubwa uongozi wake una tabia zinazofanana za kutowaamini makocha hata kama timu inafanya vizuri.

Juu ya tetesi za kusakwa kwa mbadala wa Mbelgiji huyo, imedaiwa kuwa jukumu hilo amekabidhiwa meneja wa mshambuliaji wa Simba, Meddie Kagere, anayefahamika kwa jina la Patrick Kagumba ‘Super Manager’.

BINGWA lilifanya jitihada za kumsaka meneja huyo ili kufahamu ukweli kuhusiana na tetesi hizo ambapo alikiri hilo akisema tayari yupo katika mazungumzo na makocha kadhaa wakubwa Afrika.

“Nilipigiwa simu na uongozi wa Simba kuwa wanahitaji kocha, hivyo katika harakati zangu, kuna makocha nimeona watawafaa, hivyo nipo katika mazungumzo nao,” alisema.

Kikosi cha Simba leo kitashuka dimbani kuvaana na Singida United katika mchezo utakaopigwa Uwanja wa Namfua, Singida ambao Wekundu wa Msimbazi hao wanahitaji pointi moja tu ili kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

Post a Comment

0 Comments