Windows

Simba SC yapiga hodi Zambia, Chile



ILI kunasa wachezaji wenye kiwango cha juu watakaouendeleza moto wao waliouwasha msimu huu katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba imepanga kupiga hodi nchini Zambia, Chile, Ivory Coast, DR Congo ambako wanaamini kupata ‘majembe’ hasa.

Msimu huu Simba ilifika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kutokana na kuwa na kikosi kipana chenye wachezaji wengi wazoefu wa michuano ya kimataifa kama Emmanuel Okwi, Meddie Kagere, Haruna Niyonzima, Erasto Nyoni, Aishi Manula, Clatous Chama, Jonas Mkude na wengineo.

Lakini pamoja na kuwa na wakali hao, Simba inaamini kuwa inahitaji wachezaji wenye viwango vya juu zaidi yao ambao watawawezesha kutwaa ubingwa wa michuano hiyo mikubwa kabisa kwa ngazi ya klabu barani Afrika.

Akizungumza na BINGWA juzi, mmoja wa vigogo wa ngazi ya juu Simba, alisema kuwa msimu ujao wamepania kufanya mapinduzi makubwa katika soka la Afrika na kuzipindua timu kongwe kama Al Ahly ya Misri, TP Mazembe ya DR Congo na nyinginezo.

Alisema ili kufanikisha hilo, hawatakuwa na mzaha katika suala zima la usajili na akili yao wameielekeza katika nchi hizo hapo juu, lakini pia zikiwamo Morocco na Tunisia.

“Tunashukuru kwa hatua tuliyofikia mwaka huu kwa kucheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa, kwani hatukuwa tumeitarajia. Kwa hiyo msimu ujao tunataka kufika mbali zaidi, ikiwezekana kutwaa kombe.

“Ili tuweze kutwaa ubingwa wa Afrika, tunahitaji kusajili wachezaji wa kiwango cha juu zaidi kutoka katika nchi zilizopo juu kisoka,” alisema kiongozi huyo.

Kikosi cha Simba kwa sasa kipo katika nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na kwamba iwapo kitashinda mchezo wao wa leo dhidi ya Singida United unaotarajiwa kupigwa Uwanja wa Namfua, Singida au kupata sare, watakuwa wamebeba ‘mwali’ rasmi.

Hii itakuwa ni mara ya pili mfululizo Simba kutwaa ubingwa huo iliousotea kwa misimu mitano bila mafanikio, ikiwakodolea macho watani wao wa jadi, Yanga wakibeba ‘mwali’ mara nne na Azam mara moja.

Post a Comment

0 Comments