Windows

Hesabu siku tu kumwona Samatta EPL au La Liga



KWA muda mrefu zimekuwa zikisikika taarifa za nyota wa kimataifa wa Tanzania anayeichezea KRC Genk, Mbwana Samatta, kutakiwa na klabu za Ligi Kuu ya England (EPL) au La Liga.

Pale England, Everton iliwahi kuhusishwa na mpango wa kumtaka nahodha huyo wa Taifa Stars, huku Real Betis nayo ikitajwa kwa upande wa La Liga.

Hata hivyo, tetesi hizo zilikuja kabla ya hiki alichokifanya mshambuliaji huyo hivi karibuni.

Ukiacha kuipa Genk taji la Ligi Kuu nchini Ubelgiji, ambalo haikuwahi kulibeba tangu mwaka 2011, pia amezitikisa nyavu mara 23.

Kubwa kuliko, ni kitendo chake cha kuinyakua tuzo ya Mchezaji Bora mwenye asili ya Afrika msimu huu wa Ligi Kuu hiyo, mbali ya kuwa ataweka rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kutia mguu Ligi ya Mabingwa Ulaya, wakati Genk itakaposhiriki michuano hiyo msimu ujao.

Historia inaonesha kuwa wanasoka wengi kutoka barani humu waliowahi kuibeba wakiwa Ubelgiji, walichukuliwa na klabu kubwa muda mfupi tu baadaye. Nitatolea mifano saba tu.

Daniel Amokachi, mshambuliaji huyo wa zamani wa Super Eagles, alipoinyakua 1994 akiwa na Club Brugge, alisajiliwa na Everton.

Pia, wengi watakumbuka kuwa aliyekuwa rafiki yake katika kikosi hicho, Celestine Babayaro, alipewa tuzo hiyo mwaka 1996 na miezi michache baadaye alitua Chelsea.

Ilikuwa hivyo pia kwa Vincent Kompany, ambaye ana asili ya DRC. Alipoichukua akiwa na Anderlecht mwaka 2005, ndipo alipochukuliwa na Hamburger SV ya Bundesliga aliyodumu nayo kwa miaka miwili kabla ya kutua Man City.

Haijasahaulika kuwa hata Marouane Fellaini, mwenye asili ya Morocco alipoichukua mwaka 2008 akiwa na Standard Liege, Everton walimbeba, kabla ya kutua Man United.

Ni kama ilivyokuwa kwa Romelu Lukaku, ambaye naye ana asili ya DRC. Aliibeba mwaka 2011 akiwa na Anderlecht na haikuchukua muda mrefu kabla ya kutua Chelsea.

Ukiacha huyo, yumo pia Michy Batshuayi, mwanasoka mwenye asili ya DRC aliyeichukua mwaka 2014 akiwa na Standard Liege. Muda mfupi baadaye, Marseille wakamsajili na sasa yuko pale Chelsea licha ya kucheza kwa mkopo Borussia Dortmund, Valencia na sasa Crystal Palace.

Katika orodha hiyo, nimalizie kwa kumtaja kiungo mwenye asili ya DRC anayecheza kwa mkopo Leicester City akitokea Monaco, Youri Tielemans.

Tielemans (22), alishinda tuzo hiyo mwaka juzi alipokuwa staa wa Anderlecht na ilimfungulia mlango wa kwenda Monaco.

Je, ikiwa naye ameiweka mkononi msimu huu, ni zamu ya Samatta, mshambuliaji wa zamani wa African Lyon, Simba na TP Mazembe, kunyakuliwa na klabu zenye majina makubwa katika soka la Ulaya na ulimwenguni kwa ujumla?

Huku fainali za Afcon 2019 zikiwa njiani, ambapo ataiongoza Taifa Stars huko Misri, ni wazi itakuwa ni nafasi yake nyingine ya kuthibitisha kuwa ni wakati wake kupewa tiketi ya kwenda EPL au La Liga.

Kila la heri Samatta. Kila la heri nahodha wa Stars. Kila la heri balozi wa soka la Tanzania huko ughaibuni.

Post a Comment

0 Comments