Windows

SEVILLA KUITIKISA BONGO LEO

WALE mabingwa mara tano wa taji la Europa, Sevilla, wanatarajiwa kuingia nchini leo saa 12 jioni wakitokea Hispania baada ya wikiendi iliyopita kucheza mechi yao ya mwisho ya Ligi Kuu ya nchi hiyo, La Liga dhidi ya Athletic Bilbao na kushinda mabao 2-0.
Timu hiyo iliyoweka rekodi ya kuchukua mataji mengi ya Ligi ya Europa itacheza mchezo wa kirafiki kesho kutwa dhidi ya mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba.
Ujio huo unatarajiwa kuwa na watu zaidi ya 50 huku kukitarajiwa kuwa na mambo mbalimbali tofauti na mchezo huo ambao utachezwa saa moja usiku kesho kutwa, huku kiingilio cha chini kikiwa ni shilingi 5,000.
Mkurugenzi wa Uendeshaji wa SportPesa, Abbas Tarimba, amesema kuwa ujio huo wa Sevilla umeambatana na mambo mengi ambayo yatakuwa na faida kwa Tanzania tofauti na mchezo wenyewe.
Tarimba alisema hiyo itakuwa fursa kwa timu mbalimbali za Ligi Kuu Tanzania Bara kujifunza jinsi ya kuendesha klabu zao, huku kukitarajiwa kuwa na mafunzo kwa timu ya vijana ya Bombom.
“Hii ni fursa adhimu ambayo inatakiwa kupokelewa kwa mikono miwili na timu za hapa nyumbani, kutakuwa na mafunzo mbalimbali ya jinsi ya kuendesha timu kibiashara.
“Pia, kupitia Sevilla vijana wa kituo cha kukuzia vipaji cha Bombom watapata fursa ya kujifunza huku kukiwa na baadhi ya wachezaji wa timu zote mbili, yaani Simba na Sevilla.
“Timu hiyo kutoka Hispania watafanya shughuli mbalimbali zenye lengo la kuinua sekta ya michezo nchini kwa vijana na mpira wa miguu kiujumla,” alisema.
Kuelekea mchezo huo, Msemaji wa Simba, Haji Manara, amesema kuwa kikosi chao kipo imara na tayari kwa mchezo huo ambao utaenda kuandika historia kubwa Afrika Mashariki na Kati.
Alisema kuwa licha ya ratiba ya Ligi Kuu Bara kuwabana, hawatakuwa na kisingizio chochote kuhusiana na mchezo huo.
“Tunajua umuhimu wa mchezo huo, kikosi kipo kamili na imara kwa mechi hiyo kubwa Afrika Mashariki na Kati, niwaombe mashabiki wa Simba waje kwa wingi kama walivyofanya katika michezo yetu ya kimataifa na Ligi Kuu,” alisema Manara.

Post a Comment

0 Comments