Ikiwa imebakiza mechi tatu mkononi ikiwemo ya leo, Simba inahitaji matokeo ya aina mbili tu leo ili kukamilisha hesabu na kutwaa ubingwa na kuzidi kuwakatisha tamaa wapinzani wao Yanga wanaotegemea miujiza ili waipiku na kunyakua taji hilo.
Ushindi dhidi ya Singida United utaihakikishia Simba kutetea ubingwa msimu huu kwa kuwa itafikisha pointi 91 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine inayoshiriki ligi hiyo msimu huu.
Yanga inayoshika nafasi ya pili kwa pointi 83, ikishinda mechi mbili dhidi ya Mbeya City na Azam, itafikisha pointi 89 ambazo zitakuwa mbili pungufu ya zile za Simba ikiwa itashinda leo.
Lakini ikitokea Simba ikatoka sare na Singida leo, kwa utaratibu itakuwa bado haijawa bingwa, lakini kiuhalisia itakuwa imejihakikishia taji kwani itafikisha pointi 89 ambazo ndizo zitafikiwa na Yanga ikiwa itashinda mechi zake mbili.
Ikiwa hivyo, Yanga itapaswa kutegemea miujiza ya Simba kufungwa idadi kubwa ya mabao katika mechi mbili zilizobaki dhidi ya Biashara United na Mtibwa Sugar na kisha yenyewe izifunge Mbeya City na Azam kwa idadi kubwa ya mabao ili kutwaa ubingwa kwa kuwa na uwiano mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa
Na kama uwiano wa mabao ukiwa sawa, Simba watanufaika tena ikiwa watalingana kwa idadi ya pointi na Yanga kwani watabebwa na kigezo cha tatu ambacho ni kuangalia matokeo ya mechi baina ya timu mbili zilizolingana pointi.
Katika mechi mbili ambazo zimekutanisha timu hizo, Simba ina matokeo mazuri kwani mechi ya kwanza walitoka suluhu na mechi ya pili Yanga ilichapwa bao 1-0.
Kimsingi ukiondoa hilo, jambo jingine linaloiweka Simba kwenye nafasi nzuri kisaikolojia ni rekodi yake nzuri dhidi ya Singida United ambayo ilipanda na kushiriki Ligi Kuu msimu uliopita.
Katika mechi tatu ambazo timu hizo zimekutana tangu Singida ilipopanda, Simba imeshinda michezo yote, ikifunga mabao tisa na kutoruhusu bao.
Ikiwa itatangaza ubingwa mara ya pili mfululizo kwa Simba kufanya hivyo mkoani Singida kwani mara ya kwanza ilikuwa msimu uliopita walipofanya hivyo, lakini ilikuwa kabla ya mchezo baada ya wapinzani wao Yanga kupoteza mbele ya Prisons kwa bao 1-0.
Simba leo itategemea safu yao ya ushambuliaji ambayo imekuwa moto msimu huu hasa Meddie Kagere ambaye amefunga mabao 22.
Kocha wa Simba Patrick Aussems alisema wanaingia uwanjani wakiwa na tahadhari kubwa mbele ya Singida, lakini wamejipanga kupata ushindi.
“Tunafahamu tunahitaji pointi moja, lakini wapinzani wetu wanatakiwa kupata pointi sita katika mechi mbili walizobakiza, hivyo tunahitaji kupata ushindi ili kunogesha ubingwa,” alisema Aussems.
Kocha wa Singida United, Fred Minziro alisema wanaipa heshima Simba, lakini wanalazimika kuhakikisha wanashinda ili wajinusuru na janga la kushuka daraja.
Katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyochezwa jana kwenye Uwanja wa Karume mkoani Mara, Biashara United iliichapa Mwadui ya Shinyanga mabao 2-1.
0 Comments