Kipa huyo amesema licha ya kwamba hajaonekana uwanjani kwa muda mrefu, lakini amekuwa akijifua vilivyo ili akirejea tena msimu ujao awe moto kwelikweli.
Kakolanya alimalizana na Yanga kwa kuvunjiana mkataba na amekuwa akitajwa kuwindwa na Simba ili kwenda kumpa changamoto kipa namba moja wa timu hiyo, Aishi Manula.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kakolanya alisema kuwa kwake nje kwa muda mrefu, kumemfunza mambo mengi, lakini pia amekuwa akifanya mazoezi kila siku kama alivyokuwa akiichezea Yanga na yupo fiti kinoma, huku akiwachambua wenzake.
Kakolanya alisema namna ambavyo alikuwa anafanya mazoezi kama vile anacheza kwenye kikosi cha kwanza na kudai akirejea hatapata tabu ya kuanza kwa ugumu.
“Mchezaji yeyote mwenye malengo ya kufika mbali, huwezi kuacha kufanya mazoezi, hata kama hachezi, ndio maana sipumziki kwani nina programu nimezichukulia kama sehemu ya maisha yangu,” alisema.
Aliyekuwa Kocha wa Makipa wa Simba, Idd Pazi ‘Father’ akimzungumzia Kakolanya alisema kwa uwezo alionao endapo kama msimu unaokuja atapata timu sahihi ataleta changamoto ya ushindani dhidi ya Manula katika Timu ya Taifa, Taifa Stars.
“Kwa uwezo wa Kakolanya akianza kucheza mechi za ligi itasaidia sana kwenye kikosi cha Stars, kuwepo na ushindani wa makipa kwani ana kipaji kikubwa na anajitambua anapokuwa langoni,” alisema nyota huyo wa zamani wa kimataifa.
0 Comments