Windows

Usajili wa Bocco hatari

Image result for Usajili wa Bocco hatariSTRAIKA John Bocco ameanza kutikisa mapema kwenye usajili, baada ya awali kuwepo kwa taarifa za vigogo wa Azam FC kumtengenea fuba la maana ili umrejeshe kikosini, lakini ghafla jana Ijumaa zikaibuka taarifa nyingine zikidai kuwa nahodha huyo wa Simba amesaini mkataba mpya wa miaka miwili Msimbazi wenye thamani ya Sh 80 milioni.
Hata hivyo, mabosi wa Simba wamechomoa ishu ya kumuongezea Bocco mkataba mpya kwa madai kwamba hawajaanza zoezi la usajili, huku taarifa nyingine zikidai fedha za kumpa mkataba huo hazipo kwani bilionea wao, Mohammed ‘Mo’ Dewji ndio kwanza ametua nchini juzi Alhamisi akitokea ughaibuni alipokuwa kwa mapumziko.
Taarifa za Bocco kudaiwa kusaini mktaba huo mpya Msimbazi zimekuja wakati Mwanaspoti likidokezwa kuwa vigogo wa Azam wapo kwenye mchakato wa kuyarudisha majembe yao yote yaliyotimka kikosini kwao ama kutolewa kwa mkopo kwenye klabu nyingine.
Inaelezwa mmoja wa wakurugenzi wa klabu hiyo ametenga fungu la maana ili Bocco, Shomari Kapombe na kipa Aishi Manula warejee Chamazi, lakini ghafla jana ndipo zikaibuka taarifa hizo mpya ambazo hata hivyo, viongozi wa Simba wameziruka kimanga.
Azam inapambana kuyarejesha majembe yao kutokana na kuwa na imani ya kushiriki michuano ya CAF mwakani kupitia Kombe la FA watakapocheza na Lipuli katika fainali itakayopigwa Juni Mosi, kwenye Uwanja wa Ilulu, mjini Lindi.
Hata hivyo, Mwanaspoti limepenyezewa taarifa kwamba juzi usiku baada ya mechi dhidi ya Mtibwa Sugar, mabosi wa Simba fasta waliwaita nyota waliomaliza mikataba yao ili kumalizana nao baada ya kufanya mazungumzo ya awali.
Katika mazungumzo hayo walioitwa ni John Bocco, Erasto Nyoni na Aishi Manula, lakini katika makubaliano ni Bocco na Nyoni walionyesha kukubaliana na mabosi hao wa Msimbazi.
Chanzo kutoka Simba kimesema wachezaji hao waliitwa kutokana na kuonyesha mchango mkubwa katika timu, hivyo walitaka kufahamu mipango yao kwa ajili ya msimu ujao na katika mazungumzo hayo ndipo Bocco aliyefunga mabao 15 alipokubali kumwaga wino kwenye mkataba wa miaka miwili wenye thamani inayodaiwa kufikia Sh 80 milioni.
Taarifa hizo zinasema Bocco atalamba mshahara usiopungua Sh 8 milioni, japo awali alitaka apewe Sh 10 milioni.
“Bocco ameshamalizana na Simba ndugu yangu na jamaa wamempa pesa hiyo, kwa sababu ameonyesha uwezo mkubwa sana halafu alikuwa anapata kitu kidogo tofauti na washambuliaji wenzake, kikubwa Simba inataka kuwabakiza nyota wake wote,” kilisema chanzo hicho.
Vigogo hao wa Simba walikubali kutoa pesa hizo kutokana na mshambuliaji huyo kuonyesha mchango mkubwa tangu alivyojiunga nao, huku kwa Nyoni ambaye naye alikuwa anahitajika Azam yeye aliwaambia mabosi hao kwamba hana mpango wa kurejea Azam, hivyo Simba wamuandalie ofa nzuri ili aendelee kusalia kikosini.
Kuhusu Manula inatajwa alitaja dau kubwa ambalo vigogo hao walishika vichwa na kumtajia pesa waliyoiandaa kwa ajili yake, hivyo wakamuambia akajitafakari kisha ndio waweze kukaa mezani tena, lakini Kapombe ilishindikana kwani alikuwa nje ya jiji.
VIONGOZI WARUKA
Mwanaspoti katika kuthibitisha taarifa hizo ilimsaka Mwenyekiti wa Simba, Swedi Mkwabi ambaye alisema usajili Simba haujaanza na hilo la Bocco analisikia kwa mara ya kwanza kutoka kwa mwandishi.
“Ni kweli kuna wachezaji wanaomaliza mikataba, lakini bado hatujaanza mazungumzo wala kusajili kwa vile akili zipo kwenye ubingwa wa Ligi Kuu, ila juu ya Bocco kusaini sina taarifa zozote kwa kweli,” alisema Mkwabi.
MKUDE BADO
Wakati Bocco akiwa ameshamalizana na Simba huku Kapombe na Nyoni wakiwa wanafuatia, kiungo mkabaji wa Simba, Jonas Mkude bado hajajua hatama yake ndani ya timu hiyo.
Mkude mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu pamoja na kiungo mwenzake James Kotei, lakini bado hajajua hatma yake ndani ya kikosi hiko.
Akizungumza na Mwanaspoti alisema bado hajafanya maongezi na timu yoyote lakini lolote linaweza kutokea hivi karibuni.
“Bado sijazungumza na yeyote, ila tuwe wavumilivu kila kitukuwa wazi hivi karibuni.”

Post a Comment

0 Comments