Windows

Simba yapania kuibomoa Gor Mahia



BODI ya Wakurugenzi ya Klabu ya Simba chini ya Mwenyekiti wake, Mohammed Dewji ‘Mo’, inaendelea kufanya vikao mara kwa mara ambapo sasa imepania kufanya usajili kwa gharama yoyote huku wakipanga mikakati ya kuibomoa timu ya Gor Mahia ya Kenya.

Hatua hiyo imekuja baada ya viongozi wa Simba kuridhika na kiwango cha mshambuliaji wa timu hiyo, Meddie Kagere, ambaye sasa anaongoza katika ufungaji bora akiwa amefunga mabao 23 katika michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Akizungumza na BINGWA jana, Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Simba, Crescentius Magori, alisema baada ya kuridhishwa na kiwango cha Kagere, sasa wameona nyota mwingine katika kikosi cha Gor Mahia hivyo wapo mbioni kufanya naye mazungumzo.

Alisema wataangalia na klabu nyingine kubwa barani Afrika, ila hadi sasa kuna kifaa kingine ambacho kocha mkuu wa timu hiyo, Patrick Aussems, amekipendekeza kutoka nchini humo.

“Hatufanyi usajili kwa kushindana bali tunafuata vigezo, tutaendelea kuibomoa Gor kwa mara nyingine kwani kuna mchezaji aliyependekezwa na Aussems ambaye tumemfuatilia na kujiridhisha atatufaa katika michuano ya kimataifa na ligi,” alisema.

Magori alisema mbali na Gor Mahia pia wanaangalia wachezaji katika klabu nyingine kubwa zilizofanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa, huku akisisitiza wanafanya usajili wa nyota ambao watakuwa bora zaidi ya waliopo sasa.

“Usajili utakaofanyika sasa hivi ni wa kushangaza, malengo yetu ni kutwaa taji la ubingwa Afrika hivyo itatulazimu kusajili wachezaji wenye viwango bora zaidi ya waliokuwepo ndani ya kikosi chetu kwa sasa,” alisema Magori.

Magori ni miongoni mwa viongozi waliopewa jukumu la kufanya usajili tangu msimu uliopita ambapo juhudi zake zilionekana kwa kumleta Kagere pamoja na kiungo, Clatous Chama, kutoka nchini Zambia.

Post a Comment

0 Comments