Windows

Kutinyu njia nyeupee Yanga



KIUNGO wa Azam FC, raia wa Zimbabwe, Tafadzwa Kutinyu, ameonyeshwa njia ya kutokea baada ya uongozi wa klabu hiyo kuweka wazi kutomwongezea mkataba, hivyo kuwa huru kwenda kokote, ikiwamo Yanga wanaodaiwa kumtaka.

Kutinyu, aliyesajiliwa na Azam FC msimu huu akitokea Singida United, anamaliza mkataba wake Mei 30, mwaka huu na tayari ameshatimkia nchini kwao Zimbabwe.

Akizungumza na BINGWA jana, Meneja wa Azam FC, Philip Allando, alisema wamewaongezea mikataba baadhi ya wachezaji wanaotaka wabaki na kikosi hicho msimu ujao na kwamba wale ambao hawapo katika mipango yao, wanaachana nao.

“Kutinyu mkataba wake unamalizika Mei 30, mwaka huu, ni siku chache zimebaki, lakini hayupo katika mipango yetu ya msimu ujao, hivyo yuko huru kuondoka,” alisema Allando.

Alisema wapo wachezaji wengine wanaomaliza mikataba, lakini wanasubiri ripoti ya benchi la ufundi ili kuboresha kikosi hicho kwa ajili ya msimu ujao.

Hivi karibuni Azam FC iliwaongezea mikataba mipya wachezaji wake, Yakub Mohammed, Bruce Kangwa, Donald Ngoma, Abdallah Kheri, David Mwantika na Joseph Mahundi.

Habari kutoka ndani ya uongozi wa Yanga, zinasema kuwa, Kutinyu ni miongoni mwa wachezaji wanaowapigia hesabu ili kuwasajili kwa ajili ya msimu ujao.

Post a Comment

0 Comments