Windows

Simba yaishangaza Sevilla



MABINGWA wa Ligi Kuu Bara, Simba, walionyesha kandanda safi katika mchezo wa jana usiku uliotambulika kama La Liga World SportPesa Challenge dhidi ya Sevilla kutoka Hispania licha ya kufungwa mabao 5-4 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mchezo huo maalumu wa kimataifa wa kirafiki chini ya udhamini wa kampuni ya michezo ya kubahatisha, SportPesa, ilionyeshwa mubashara na DSTV kupitia chaneli yao ya SuperSport.

Simba walianza kwa kasi mchezo wa jana na nusura wapate bao la kuongoza dakika ya pili lakini mpira wa kichwa uliopigwa na Clatous Chama kufuatia krosi ya Emmanuel Okwi ilitoka nje.

Juhudi za Simba kulisakama lango la Sevilla zilizaa matunda dakika ya 11 baada ya kazi nzuri ya Meddie Kagere katika winga ya kulia kumtoka beki wa Sevilla na kumtengenezea pasi nzuri nahodha John Bocco aliyekwamisha mpira wavuni kwa mguu wake wa kulia.

Dakika tano baadaye, Simba walipata bao la pili likifungwa na Kagere aliyetumia makosa ya beki wa Sevilla kurudisha mpira kwa kipa wake Juan Soriano.

Sevilla walizinduka baada ya mabao hayo mawili ya haraka haraka na kusuka mipango ya kusawazisha ambapo walifanikiwa dakika ya 23. Bao hilo lilitokana na mpira wa kona kufuatia kipa Aishi Manula kupangua shuti la Nolito. Lakini mpira wa kona ulifungwa na

Sergio Escudero.

Bocco mara nyingine tena aliipatia Simba bao la tatu dakika ya 32 baada ya shambulizi la kushutukiza na mpira kumkuta Kagere ambaye alimtengea pande nzuri mfunguaji wa bao la tatu.

Simba waliendelea kucharuka na katika dakika ya 40, Jonas Mkude alikokota mpira na kufumua shuti lililotoka nje kabla ya mpira wa kichwa uliopigwa na Nolito kuokolewa na Manula. Wissam Ben Yeder ambaye alikuwa kimya muda alipata nafasi dakika ya 41 na kufumua shuti lililotoka nje.

Sevilla walirudi kwa kasi kipindi cha pili na kufanikiwa kupata bao la tatu dakika ya 50 lililofungwa na Nolito akiitendea haki pasi ya Bryan Gil. Lakini dakika 11 baadaye, Chama aliipatia Simba bao la nne iliyotokana na pasi iliyoanzia kwa Mkude kisha ikamkuta Nicholas Gyan aliyempa mpira Bocco kabla ya kumkuta mfungaji.

Mabadiliko yaliyofanywa na makocha wote wawili yalionekana kuipa nguvu zaidi Sevilla kuliko Simba ambapo wageni hao walipata bao la tatu dakika ya 85 iliyofungwa na Quincy Promes akimalizia shuti la Munir El Haddadi ambalo kipa Deogratius Munishi alishindwa kuokoa.

Promes alifunga tena bao lake la pili na nne kwa Sevilla ikiwa ni la kusawazisha dakika ya 90 baada ya kupokea pasi ya Nolito na Nolito kuhitimisha ushindi mzuri kwa Sevilla dakika za majeruhi.

Post a Comment

0 Comments