Windows

KISHINDO YANGA SC




Yanasa vifaa vya nguvu kutoka mataifa saba, kazi ipo Ligi Kuu Bara msimu ujao

YANGA imepiga hodi katika mataifa saba yaliyopo juu kisoka na kuvuna vifaa vya nguvu ambavyo vitaanza kuingia nchini muda wowote kuanzia sasa tayari kumalizana nao.

Baada ya kutofanya vizuri msimu uliopita na huu na hivyo kujikuta ikishindwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara walioushikilia kwa misimu mitatu mfululizo, yaani 2014/15, 2015/16 na 2016/17, Yanga inajipanga kuja kivingine msimu ujao.

Kwa misimu hii miwili, yaani 2017/18 na 2018/19, Simba ndio walioibuka kidedea, huku Yanga wakibaki kuwa wasindikizaji katika ligi hiyo.

Mbali ya Ligi Kuu Bara, hata katika michuano ya kimataifa, Yanga imeshindwa kufurukuta, huku Simba wakifanya kweli kwa kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, hiyo ikiwa ni rekodi ya kipekee kwa timu za Tanzania.

Ni kutokana na kudorora kwa timu yao ndani ya misimu hii miwili, lakini pia kitendo cha Simba kutamba Afrika, Yanga chini ya uongozi mpya uliochaguliwa hivi karibuni wanajipanga upya ili kurejesha makali yao na hata kujibu mapigo ya watani wao hao wa jadi kimataifa.

Na kati ya mikakati ya uongozi huo wa Yanga, chini ya Mwenyekiti wake, Dk. Mshindo Msolla, ni kusajili wachezaji wa kiwango cha juu, zaidi ikiwa ni kutoka nje ya Tanzania.

Akizungumza na BINGWA jana, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela, amewataka mashabiki wao kukaa mkao wa kula kupokea vifaa vya nguvu.

“Tumeingia madarakani kwa ajili ya kuwapa raha mashabiki na wanachama wetu, kuanzia sasa tunategemea kuanza kuwapokea wachezaji wetu wa kigeni,’’ alisema Mwakalebela.

Mwakalebela aliyataja mataifa wanayotoka wachezaji hao kuwa ni DR Congo, Ivory Coast, Nigeria, Ghana, Zambia, Rwanda na Burundi.

Kuhusu majina ya wachezaji hao, Mwakalebela alisema ni mapema sana kuyaweka hadharani, lakini iwapo mambo yatakwenda kama yalivyopangwa, huenda leo baadhi yao wakaanza mazoezi kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi kilichopo Kurasini, jijini Dar es Salaam.

“Kama unavyojua, ukianza kutaja majina, itakuwa shida kidogo kwa wenzetu wa upande wa pili. Niamini kwamba tunashusha vifaa vya nguvu. Mwakani kazi itakuwa ni moja tu, kutoa vipigo kwa kila atakayekuja,’’ alisisitiza Mwakalebela.

Pamoja na kuongoza Ligi Kuu Bara msimu huu kwa muda mrefu, Yanga imeshindwa kufurukuta mbele ya Simba, waliokuwa na kikosi kipana na chenye nyota wazoefu, wakiwamo Emmanuel Okwi, Meddie Kagere, Pascal Wawa, Erasto Nyoni, John Bocco na wengineo.

Post a Comment

0 Comments