


STRAIKA wa Yanga, Heritier Makambo, raia wa DR Congo, anatarajia kwenda kuanza maisha mapya ndani ya timu ya Horoya AS ya Guinea, huku akiacha rekodi adimu mno Jangwani.
Makambo, aliyeitumikia Yanga kwa msimu mmoja, alisaini mkataba wa miaka mitatu na klabu hiyo ya Guinea hivi karibuni kwa dau la zaidi ya Sh milioni 200.
Kuondoka kwa Makambo Yanga kumezua maswali mengi kwa Wanayanga, hasa kutokana na mchango wake kwa timu hiyo, akifunga mabao 17 katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mbali ya uwezo wake wa kufunga mabao, Makambo anaondoka Yanga akiwa ameweka rekodi ya kipekee kwa kukosa mchezo mmoja tu wa Ligi Kuu Bara hadi juzi, tofauti na ilivyo kwa wachezaji wote wa kikosi hicho msimu huu.
Mchezo aliokosa ni dhidi ya JKT Ruvu, uliopigwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, kutokana na kutumikia adhabu ya kadi tatu za njano.
Pia Makambo ni mchezaji ambaye hajawahi kukosa mazoezi ya Yanga, kuonyesha jinsi alivyokuwa na nidhamu ya hali ya juu pamoja na klabu hiyo kuwa na hali ngumu ya kiuchumi.
Mratibu wa Yanga, ambaye muda wote ndiye anayeshughulikia masuala ya mahudhurio ya wachezaji na kupokea taarifa zao mbalimbali, Hafidh Saleh, amethibitisha hilo.
Alisema kwa kipindi chote alichokaa na Makambo, amebaini ni mchezaji mwenye tabia za pekee na inawezekana ndicho kilichomfanya apate ofa haraka.
“Makambo hajawahi kukosa mechi kwa kuumwa, muda mwingi alikuwa fiti, akifanya mazoezi kwa kujituma na kuzingatia muda, pia ana nidhamu ya hali ya juu.
“Licha ya kufanya vizuri uwanjani, pia amekuwa na ushirikiano mkubwa na wenzake, bila kujali umri na amekuwa akizingatia kila kitu anachoelekezwa,” alisema Saleh.
Saleh amemfananisha Makambo na wachezaji wao wawili wa zamani waliochezea Yanga, ambao ni Simon Msuva na Boniface Ambani.
“Wachezaji waliowahi kucheza Yanga ninaoweza kuwafananisha na Makambo ni Ambani na Msuva, kutokana na nidhamu na kujituma,” alisema.



0 Comments