Windows

Serikali yaitaka TFF ibadilike


Serikali imelitaka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuacha kufanya kazi zake kwa upendeleo ili kuharakisha maendeleo ya mchezo huo

Hayo yalisemwa jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo wakati akifunga semina ya Maafisa Michezo nchini iliyokuwa inafanyika jijini Dodoma

Waziri Jafo alisema hakuna sababu ya shirikisho hilo kuendekeza "majungu" kwa maslahi yao wenyewe, na kama wataendelea na mfumo huo watakuwa wanashiriki kuua soka la nchi.

Jafo alisema endapo kutakuwa na vitendo vya upendeleo, jambo hilo litakatisha tamaa wachezaji wa timu nyingine licha ya kuwa na uwezo wa kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali wanayoshiriki.

Waziri huyo alisema kuwa timu za hapa nchini zinafanya vema katika mechi zake mbalimbali licha ya kukabiliwa na tatizo la ukata lakini zimekuwa zikijitahidi kupambana hadi katika michezo yake ya mwisho ya msimu.

Aliipongeza Yanga iliyokuwa inachuana na klabu "tajiri" (hakuzitaja)kwa kushika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu licha ya kuwa na matatizo ya fedha.

"Yanga ilikuwa kama mtoto yatima mwenye njaa lakini akiingia darasani anafanya vizuri, Yanga imesumbua sana kwenye ligi na inastahili pongezi kwa sababu imepambana na watoto wanaokula mkate kwa blueband," alisema Jafo.

Aliwataka TFF kujitathmini na kuacha kufanya kazi bila ya kufuata kanuni na taratibu na kuweka mbele maslahi ya timu zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara

Post a Comment

0 Comments