


MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba, wamefanikiwa kutetea ubingwa wao baada ya kuifunga mabao 2-0 Singida United katika mchezo uliochezwa juzi kwenye Uwanja wa Namfua, mkoani Singida.
Simba wametetea ubingwa wao wakiwa bado wanamichezo miwili mkononi baada ya kucheza michezo 36 na kufikisha pointi 91 ambazo hazitafikiwa na timu nyingine yoyote.
BINGWA tuna kila sababu ya kuipongeza Simba, lakini tukiungana na wadau wengine wa soka kwa klabu hiyo kufanikiwa kutetea ubingwa wao.
Tunaamini kuwa Simba wamefanikiwa kutimiza malengo yao kutokana na maandalizi yaliyofanywa kuanzia usajili wa wachezaji, benchi zuri la ufundi na uongozi kwa ujumla.
Hivyo basi, ubingwa wa Simba uwe ni mwanzo wa maandalizi ya michuano mingine ikiwamo Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo inashinda makali.
BINGWA tunasema mafanikio ambayo Simba wanapata kwa miaka miwili sasa yanatokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa ndani ya klabu hiyo.
Tunasema kuwa juhudi za Simba kufanya vizuri zisiishie michuano ya ndani, hivyo wanahitaji kuangalia zaidi na ile ya kimataifa.
BINGWA tunasema kuwa kiu ya mashabiki wa Simba na Watanzania kwa ujumla ni kutaka kuona Kombe la Afrika linatua nchini baada ya mwaka huu Simba kuishia hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Tunaamini kwamba, Simba wakianza kujipanga mapema kwa kusajili wachezaji wenye uwezo wa hali ya juu kimataifa, wataweza kuitangaza vyema Tanzania katika anga za kimataifa.
Tunahitaji kuona Simba bora zaidi ya msimu huu ambayo ilisheheni nyota wengi wakiwamo wa kigeni kama Emmanuel Okwi, James Kotei, Haruna Niyonzima, Pascal Wawa, lakini wazawa John Bocco, Erasto Nyoni, Aishi Manula na wengineo.
Kama tulivyosema michuano ya kimataifa inakuwa na ushindani mkali, hivyo itakuwa ni vizuri zaidi kwa benchi la ufundi la Simba na uongozi wa klabu hiyo, kuangalia mapungufu yaliyojitokeza katika kikosi chake na kuyafanyia kazi kabla msimu mpya kuanza baadaye.
Tunarudia kuipongeza Simba kwa kutwaa taji kwa mara nyingine mfululizo, lakini wasibweteke na mafanikio ya ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwani wajipange zaidi ili waweze kufanya vyema kimataifa



0 Comments