MEDDIE Kagere wa Simba ameshikwa na kigugumizi alipotakiwa kumtaja mchezaji ambaye hakutamani kumkosa kikosini mwao katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara na za Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.
Kagere ndiye aliyeibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara, akicheka na nyavu mara 23 kuiwezesha timu yake kutetea ubingwa wao kwa kufikisha pointi 93, baada ya kucheza mechi 38.
Mshambuliaji huyo raia wa Rwanda, alichangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya Simba msimu huu, huku akipata ushirikiano wa hali ya juu kutoka kwa nyota wenzake, akiwamo Emmanuel Okwi, John Bocco na wengineo.
Akizungumzia mafanikio yake msimu huu, Kagere alisema kama si ushirikiano kutoka kwa wenzake, hadhani kama angeweza kutwaa tuzo ya mfungaji bora.
“Mafanikio yangu yalitokana na utendaji wa timu nzima, kuanzia kwa wachezaji wenzangu pamoja na benchi la ufundi. Haikuwa nguvu au uwezo wa mtu mmoja mmoja,” alisema.
Alipoulizwa ni mchezaji gani ambaye hata siku moja hakutamani kumkosa kikosini mwao, Kagere alishindwa kumtaja yeyote, akiwamo Okwi ambaye ni miongoni mwa vipenzi vya Wanamsimbazi.
“Daa, hapo sina la kusema, mimi naona wote walikuwa na nafasi sawa katika mafanikio ya timu, kila mmoja aliipigania timu ili ipate matokeo na si kuangalia mafanikio binafsi,” alisema. Kagere alitua Simba msimu huu akitokea Gor Mahia ya Kenya, ambapo Wekundu wa Msimbazi hao walimwona katika michuano ya SportPesa mwaka jana iliyofanyika katika taifa hilo linaloongozwa na Rais Uhuru Kenyatta.
0 Comments