Windows

Okwi aipasua kichwa Simba


STRAIKA wa Simba, Emmanuel Okwi ameigawa Simba ikiwa ni saa chache tangu atupie ujumbe kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii akionyesha kama anayeaga.


Hata hivyo, upande wa viongozi ni kama vile wamempa mkono wa kwaheri wakisisitiza kama ndio anasepa, basi asepe zake salama kwani hawana mpango naye ndio maana mpaka sasa hawajafanya mazungumza naye.


Okwi aliyeichezea Simba takribani misimu sita tofauti tangu mwaka 2010 kwa misimu miwili ya mwisho ukiwamo huu unaomalizika leo, amefunga jumla ya mabao 36 ya Ligi Kuu mbali na yale ya michuano mingine.


Katika ujumbe wake wa Instagram ni kama mtu anayeaga, japo mwenyewe alidai ujumbe huo umetokana na mistari ya nyimbo moja matata, lakini tayari wadau wa soka na hasa wa Simba wamegawanyika wengine wakitaka aongezewe mkataba.


Mwenyekiti wa Simba, Swedi Mkwabi alisema, Okwi kama anaondoka hawana tatizo, kwani hawajafanya naye mazungumzo yoyote mpaka sasa juu ya mkataba mpya, jambo lililoungwa mkono na nyota wa zamani wa klabu hiyo, Zamoyoni Mogella.


Mogella alisema kama taarifa za Okwi kuondoka ni kweli haitakuwa tatizo kwani Simba inaweza kumsajili mchezaji mwingine mwenye uwezo wa kuziba nafasi yake.


Mkongwe huyo alisema ni Okwi anaondoka akiwa na kiwango kizuri, lakini viongozi wa Simba wanapswa kuwa makini kufanya usajili mzuri ili kuleta mbadala wake ambaye moja kwa moja ataingia kwenye timu na kufanya kazi zaidi yake.


“Simba wamepita wachezaji wengi kama Abdallah Kibadeni na wengineo wengi, hivyo kuondoka kwa Okwi sio ishu sana muda wake umeshafika wa kuondoka akiwa na heshima, lakini lazima aletwe mkali zaidi yake kuziba nafasi.”


Naye mchambuzi na kocha maarufu nchini, Kennedy Mwaisabula alisema kama kweli Okwi ataondoka katika kikosi cha Simba litakuwa pigo kwa maana mchezaji huyo ni mzoefu wa mashindano ya ndani na Ligi ya Mabingwa Afrika.


Mwaisabula alisema misimu miwili Okwi aliyokuwa Simba amekuwa msaada kwa kutoa mchango mkubwa uliowapa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara mbili.


“Binafsi nafuatilia soka kwa karibu mno na kama Simba itamuacha Okwi sitafurahia kabisa kutokana na uzoefu na msaada wake, viongozi walitakiwa kukaa naye ili wazungumze na kukubaliana katika maslahi ili mpira wake aumalizie hapo,” alisema Kocha Mwaisabula.


Post a Comment

0 Comments