


WAKATI straika Obrey Chirwa akifichua kuwa yupo mbioni kutua Bidvest Wits ya Afrika Kusini, inaelezwa kigogo mzito wa Azam FC, ameingilia kati suala la usajili wa klabu hiyo akijiandaa kumshusha nyota wa Nkana FC ya Zambia, Ronald Kampamba.
Mwanaspoti limepenyezewa taarifa kigogo huyo anataka Azam isajili mchezaji wa kariba ya Kipre Tchetche ambaye aliibeba Azam katika mechi za kitaifa na kimataifa kwa umahiri wake wa kutupia na kuzikimbiza timu pinzani.
Chanzo hicho kimesema kigogo huyo ambaye ndiye tajiri wa Azam ameanza na mchezaji huyo akiomba atumiwe video zake ili aweze kuona uwezo wake wa kufunga huku akiweka wazi yupo tayari kumsajili kwa dau lolote lengo ni kuona klabu yake iingie katika rekodi za upachikaji wa mabao kama misimu iliyopita.
“Tajiri hajafurahishwa na safu ya ushambuliaji kushindwa kuwa na ushindani na imekuwa sawa na timu ambazo hazijafanya usajili mkubwa na ameomba video za Kampamba ambaye ndiye mchezaji wa kwanza kupendekezwa na baadhi ya viongozi,” kilisema chanzo.
“Bado anaendelea kufuatilia lakini amesisitiza aachiwe safu ya ushambuliaji asajili mwenyewe nyota anaoamini wataleta changamoto kwa wapinzani kama alivyokuwa Kipre Tchetche.”
Inaelezwa kigogo huyo anamtaka Kampamba na nyota wengine ambao amepanga kuwasajili Chamazi, baada ya washambuliaji waliopo sasa kama Donald Ngoma na Obrey Chirwa kushindwa kutamba.Kama Kampamba atatua Azam basi atapishana na Chirwa aliyeamua kuvunja ukimya kwa kudai sio kweli kama anataka kutua Msimbazi, ila anadili nzito la kutakiwa na Bidvest Wits ya Afrika Kusini.
Akizungumza na Mwanaspoti, Chirwa aliyesajiliwa Azam kwenye dirisha dogo msimu huu, alisema mengi yamezungumzwa, lakini habishani na mtu kwani bado ni mchezaji wa Azam, japo kuna ofa ya kucheza soka Afrika Kusini.
“Nimehusishwa na Simba msimu ujao na watu walivuka mipaka zaidi wakidai nimegoma kusaini mkataba mpya Azam, kitu ambacho si kweli mimi na klabu tumekubaliana kukaa mezani mara ya ligi ikimalizika hicho ndicho kinatakiwa kifahamike na wengine,” alisema.
“Juu ya ofa mpaka sasa ipo moja tu ya Bidvest Wits ya Afrika Kusini, ila bado sijaamua kama niende huko ama la,” alisisitiza Chirwa.



0 Comments