Windows

ZAHERA ABAKIZA 11 TU YANGA



KOCHA Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, amesema wachezaji 11 pekee kati ya 30 ndio watakaosalia katika kikosi chake cha msimu ujao, huku wengine waliokuwapo kundini ‘wakienda na maji’.

Zahera ametoa kauli hiyo wakati leo kikosi chake kikifunga msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2018/19 kwa kuvaana na Azam kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Akizungumza na BINGWA jana baada ya mazoezi ya timu yake kwenye Uwanja wa Uhuru, Zahera alisema majina ya wachezaji hao yatajulikana rasmi kesho.

“Wachezaji 11 pekee ndio watapewa mikataba mipya na waliobaki watakwenda kutafuta maisha sehemu nyingine, kujua majina subiri tumalize mechi ya kesho (leo) dhidi ya Azam.

“Kabla sijaondoka Jumatano, nitakuwa nimewasajili wachezaji wote ambao wataendelea kuwepo msimu ujao, tunasubiri tumalize mechi na Azam halafu tutatangaza majina,” alisema.

Alisema katika kikosi chake, wachezaji 17 wamemaliza mikataba yao na wengine ambao bado lakini hawapo katika mpango wao wa msimu ujao, watawatoa kwa mkopo kwingineko.

Alisema kuwa wachezaji hao 11 watakaobaki, wataungana na wengine wapya wanaoendelea kutua Jangwani ili kuunda kikosi cha mauaji kitakachorejesha heshima yao msimu ujao.

Tayari uongozi wa Yanga umemhakikishia Zahera kupewa fedha za kusajili mchezaji yeyote yule na kwa gharama yoyote, lakini akipewa masharti ya kuhakikisha hachezi kamari katika mchakato huo.

Akizungumza na BINGWA jana, Mwenyekiti wa Yanga, Dk. Mshindo Msolla, alisema: “Msimu ujao hatutaki visingizio, tumempa nafasi Zahera kusajili wachezaji anaowataka na ametuhakikishia wote wa kigeni ni wazuri wapo katika timu zao za taifa, kama timu ikifanya vibaya atawajibika,” alisema Msolla.

Katika hatua nyingine, beki Kelvin Yondani, ameshusha presha ya mashabiki wa Yanga baada ya jana kutokea kwenye mazoezi ya timu hiyo.

Yondani alikosekana katika mchezo uliopita wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Mbeya City ambapo Kocha Zahera alidai beki huyo aliwazimia simu viongozi wa timu hiyo.

Alipoulizwa na BINGWA juu ya hilo, hasa kitendo cha kuwazimia simu viongozi wake, Yondani alibaki kucheka na kudai hayo yamekwisha.

Post a Comment

0 Comments