


USHINDI wa mabao 2-0 dhidi ya Mbao katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, umempa matumaini kocha wa timu ya KMC, Etienne Ndayiragije, kumaliza nafasi nne za juu.
Timu hiyo kwa sasa inashika nafasi ya nne katika msimamo wa ligi kutokana na pointi 52, baada ya kucheza michezo 37, wakisalia na mchezo mmoja.
Akizungumza na BINGWA jijini hapa juzi, Ndayiragije alisema kwa kumaliza katika nafasi hiyo watakuwa wamevuka malengo waliyojiwekea.
Ndayiragije alisema tangu kuanza kwa msimu walipanga kucheza vyema ili wasishuke daraja, lakini kumaliza nafasi nne za juu ni bonasi kwao na ni jambo la kujipongeza.
Alisema baada ya kumaliza msimu atawaachia mipango viongozi wa klabu hiyo ili waje na mipango mikubwa zaidi kama wanatahitaji kufanya vyema zaidi msimu ujao.
Ndayiragije alisema wanahitaji kuongeza nguvu kubwa zaidi kwa msimu huu ujao.
“Mipango ya klabu ilikuwa tusishuke daraja walau tutafute nafasi ya saba, lakini kulingana na matokeo tunayoyapata sasa tumejipa morali na matumaini kwamba tunaweza kumaliza katika nafasi ya nne.
“Tunasubiri uongozi tuone sasa umejipangaje kwa msimu ujao, mipango sijui ikoje lakini kama tunahitaji kufika mbali basi lazima tutumie nguvu zaidi ya hapa,” alisema Ndayiragije.



0 Comments