Windows

Mwakalebela: Nitasajiri kikosi cha heshima

Mwakalebela

UCHAGUZI Mkuu wa Yanga umemalizika usiku wa kuamkia juzi Jumatatu kwa wagombea waliokuwa wakiwania nafasi mbalimbali za uongozi ikiwemo ya mwenyekiti, makamu na wajumbe nane kuibuka vinara.

 

Katika uchaguzi huo uliofanyika kwenye Ukumbi wa Bwalo la Maofisa wa Jeshi la Polisi, Oysterbay jijini Dar es Salaam, mgombea wa nafasi ya mwenyekiti, Dk. Mshindo Mbette Msolla ndiye aliyefanikiwa kushinda nafasi hiyo kwa kura 1,276 dhidi ya 60 za mshindani wake, Dk. Jonas Tiboroha.

 

Fredrick Mwakalebela aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), yeye alishinda kwa kuwa makamu mwenyekiti akishinda kwa kishindo kwa kujikusanyia kura 1,206 akiwashinda Janneth Mbene aliyepata kura 61, Titus Osoro kura 17, Yono Kevela kura 31 na Salum Chota Chota kura 12.

 

Baada ya uchaguzi huo, Championi Jumatano, limefanya mahojiano maalum na Mwakalebela na kuelezea mikakati na malengo yake baada ya kushinda katika nafasi hiyo. “Nianze kwa kuwashukuru wanachama wa Yanga kwa kuniamini na kunipa dhamana ya kuiongoza klabu kubwa kama hii, sikutegemea kushinda kwa idadi ya kura nyingi kama hivi.

 

“Idadi hii ya kura nyingi nilizozipata inanipa mtihani mkubwa kwa maana ya kuifanyia vitu vingi Yanga vitakavyoiondoa hapa ilipo na kuipeleka sehemu nyingine nzuri. “Hivyo, baada ya wanachama hao kunichagua, niwaahidi Wanayanga kuifanyia mambo mengi kwa kushirikiana na mwenyekiti wangu Msolla na wajumbe wapya tuliochaguliwa pamoja.

 

AVUNJA KAMBI ZA WAGOMBEA

“Lipo wazi, kambi za wagombea zilikuwa zipo nyingi katika kipindi cha uchaguzi na hiyo yote katika kuhakikisha kila mmoja anashinda uchaguzi na kuingia kuiongoza Yanga. “Binafsi nisingependa kuona kambi hizi zikiendelea ndani ya Yanga, uchaguzi tayari ushamalizika na ninaahidi kuvunja kambi na utimu na hilo litafanyika mara baada ya kukutana na viongozi wangu wapya kwa maana ya mwenyekiti na wajumbe wapya. “Hakuna ugumu kuziua kambi hizo, sisi wote wamoja hivi sasa baada ya uchaguzi huu na kilichopo ni kuungana na kuweka mikakati thabiti itakayoijenga Yanga imara.

 

AANZA NA AHADI YA KUMUWEZESHA ZAHERA KUPATA FEDHA YA USAJILI

“Kabla ya uchaguzi niliahidi kuweka mikakati thabiti ya kumuwezesha kocha wetu Zahera (Mwinyi) kupata fedha itakayotumika kwa ajili ya kufanya usajili wa kisasa. “Hivyo, katika kuhakikisha ninalitekeleza hilo kwa kushirikiana na viongozi wenzangu wapya kutafuta udhamini wa fedha kwa haraka atakazozitumia kocha wetu kwa ajili ya kusajili, hilo ndilo tutakaloanza nalo.

AAHIDI USAJILI WA UTAKAOVUNJA REKODI AFRIKA

“Ninataka kutengeneza timu yenye ushindani wa kuchukua makombe yote tutakayoshiriki Yanga kwa kuanzia ubingwa wa ligi na Kombe la Shirikisho ambalo leo (juzi) tunatarajiwa kucheza na Lipuli FC katika hatua ya nusu fainali.

 

“Usajili ninaoutaka wa kuvunja rekodi kwa kuanzia Afrika Mashariki na Magharibi, kikubwa ninataka kuiona Yanga yenye kikosi kipana cha wachezaji kwa kuanzia wale wa kikosi cha kwanza na wale wa akiba wote wawe wazuri.

 

“Tunafahamu haitakuwa rahisi, lakini kwa kushirikiana na viongozi wenzangu ninaamini nitafanikiwa na hilo linawezekana kabisa, kwani tuna kocha mzuri atakayependekeza usajili wa wachezaji wapya.

 

“Binafsi nina vitu vingi vya kuifanyia Yanga ikiwemo kuchukua ubingwa wa ligi, tunajua wenzetu wamefanya mengi hadi kufikia kuongoza ligi, hivyo kilichobaki sisi kumalizia hapo walipoishia.

 

KUUKARABATI UWANJA WA KAUNDA

“Nina malengo mengi niliyopanga kuyafanya, kati ya hayo ni kutengeneza mfumo thabiti wa kuboresha miundombinu ya klabu, yakiwemo majengo na Uwanja wa Kaunda na kupanga kujenga uwanja mkubwa wa kisasa utakaokuwa na hosteli za wachezaji. “Ninataka kuona Yanga inamiliki uwanja wake wa mazoezi utakaokuwepo kwenye makao makuu ya klabu pale Jangwani na hiyo itasaidia kupunguza matumizi ya kukodisha uwanja ambayo hivi sasa yanatumika kwa kuwa na uwanja wetu wenyewe wa mazoezi. AITISHA

 

MKUTANO MKUU WA WANACHAMA

“Ninafahamu mashabiki wa Yanga wanataka kuona klabu yao inakwenda kwenye mfumo mpya wa uendeleshaji wa klabu yao, hivyo huu ni muda muafaka wa sisi kuleta mabadiliko kwa haraka. “Hivyo, nimepanga hivi karibuni kukutana na viongozi wenzangu kwa ajili ya kuzungumza mambo kadhaa ya kuweka mipango sawa na kati ya hiyo ni kuitisha Mkutano Mkuu wa Wanachama wa Yanga utakaojadili suala hilo la mabadiliko na kama likipitishwa, basi kama watendaji tutafanya mabadiliko ya haraka,” anamaliza Mwakalebela.

 

 

The post Mwakalebela: Nitasajiri kikosi cha heshima appeared first on Global Publishers.


Post a Comment

0 Comments