Windows

Makambo, Meddy Kagere vitani upyaaa

ACHANA na presha kubwa waliyonayo Yanga kule mjini Musoma, unaambiwa kuna vita mpya inaendelea kwenye miji miwili tofauti kati ya mastraika Meddie Kagere na Heritier Makambo ambao leo Ijumaa watashuka viwanjani kuzitetea timu zao katika mechi za Ligi Kuu Bara.
Presha kubwa ipo kwa Yanga huko Musoma kwani ikiruhusu Biashara iibuke na ushindi kwenye mchezo wa leo, itakuwa ni kama imeirahisishia Simba kutetea taji, lakini kama Kagere atatupia tena ina maana, Makambo wa Yanga hatakuwa na chake msimu huu.
Timu yake imeshatolewa Kombe la FA na pia ubingwa wa Bara ni nadra kuupata, basi hata Tuzo ya Mfungaji Bora nayo aikose na hapo ndipo mashabiki watakaofuatilia mechi za watani hao watatupia macho na masikio Mara na jijini Dar wakati Simba ikiikaribisha Kagera Sugar.
Kagere ana mabao 20 kwa sasa huku Makambo akiwa na 16 akilingana na Salim Aiyee, wakifukuziwa kwa karibu na Emmanuel Okwi na John Bocco wote wa Simba wakiwa na mabao 14 kila mmoja.
Pamoja na rekodi nzuri iliyonayo dhidi ya Biashara, Yanga ni wazi inafahamu haipaswi kuingia kiwepesi kwenye mchezo huo kwa sababu mechi zote mbili ambazo ilikutana na Biashara United na kupata ushindi, zilikutana na upinzani mkali.
Yanga ilishushwa na Simba katika uongozi wa Ligi Kuu na sasa ipo nafasi ya pili na alama zake 80, moja pungufu za Wekundu wa Msimbazi na matokeo yoyote ya kupoteza kwao ni kuwapa ujiko wapinzani wao.
Timu hizo zilikutana mara ya kwanza katika Ligi Kuu, Yanga ikiwa mwenyeji na kushinda 2-1, ila ililazimika kutoka jasho kwani ilitanguliwa huku Biashara ikionyesha kiwango bora.
Kama haitoshi zilikutana tena kwenye Kombe la FA na mchezo kuisha kwa sare ya 2-2 ndani ya dakika 90 na kuamriwa kwa mikwaju ya penalti na Yanga kushinda kwa 5-4.
Katika mchezo wa leo, Yanga itamkosa nahodha wake, Ibrahim Ajibu aliyeugua ghafla muda mfupi kabla ya kusafiri, ila kiungo Rafael Daud aliyekosa mchezo uliopita dhidi ya Lipuli na kupoteza 2-0 atakuwapo uwanjani kusaidiana na Makambo na Amissi Tambwe.
Wakati Yanga ikiwa na kibarua huko Musoma, Simba iliyo kwenye mwendelezo wa matokeo mazuri itakuwa kibaruani mbele ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Uhuru jijini.
Ni mechi ambayo bila shaka Simba itaingia ikiwa na nia ya kulipa kisasi baada ya timu hiyo kugeuka kuwa mtemi wao kwa kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja sasa.
Kuanzia mwaka 2018 hadi sasa, Simba imegeuka mnyonge kwa Kagera ambapo imekutana na timu hiyo mara mbili na kupoteza zote.
Mbaya zaidi, mechi ya kwanza ambayo Simba ilicheza dhidi ya Kagera kati ya hizo mbili, ulikuwa ni ule wa Mei 18, mwaka jana ambao ilichapwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Taifa jijini mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dokta John Magufuli.
Lakini Kagera ilidhihirisha ubabe wao kwa kuibuka na ushindi pindi timu hizo zilipokutana tena Aprili 20, mwaka huu, Simba ilichapwa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Kaitaba.
Kagera italazimika kufanya kazi ya ziada kuizuia Simba ambayo imepata ushindi kwenye mechi saba mfululizo za Ligi Kuu tena tano zikiwa za ugenini dhidi ya Alliance, KMC, Biashara United, Prisons na Mbeya City na imeshinda mbili nyumbani dhidi ya JKT Tanzania na Coastal Union.
Safu ya ulinzi ya Kagera Sugar ndio inayopaswa kuwa makini zaidi katika kuikabili safu ya ushambuliaji ya Simba itakayoongozwa na Kagere, Emmanuel Okwi na John Bocco aliyepona majeraha, ambayo katika mechi hizo saba imefunga jumla ya mabao 18.
Kocha wa Simba, Patrick Aussems alisema anafurahia kiwango cha timu yake.
“Naridhika na kiwango cha timu katika siku za hivi karibuni na kama mnavyoona kwa sasa timu imeimarika na inapata matokeo mazuri licha ya ratiba ngumu tunayokabiliana nayo.
“Tunaingia kwenye mechi dhidi ya Kagera Sugar tukiwa na hesabu na malengo ya kusaka pointi tatu ili tujiweke pazuri na kutwaa ubingwa,” alisema kocha huyo anayetokea Ubelgiji.

Post a Comment

0 Comments