Windows

Kakolanya freshi, kutua Simba kiulaini

KUSHINEI. Ile filamu tamu ya muda mrefu juu ya sakata la kipa wa Yanga, Beno Kakolanya dhidi ya klabu yake, limemalizika baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuingilia kati na kutoa uamuzi wa kipa huyo kuwa huru na sasa anaweza kutua hata Simba kiulaini.
Kamati ya Sheria, Katiba na Hadhi ya wachezaji iliyokuwa inashughulikia ishu ya kipa huyo aliyetibuana na mabosi wake kwa kususia timu kabla ya kocha wake, Mwinyi Zahera kumfungia vioo, imemaliza mchezo kwa kumruhusu Kakolanya kwenda popote sasa.
Ipo hivi. Baada ya Kakolanya kupeleka barua kamati hiyo, kulikuwa na ukimya mrefu huku kipa huyo akiwa hapokei mshahara wowote kutoka Jangwani, lakini kamati hiyo ilikutana juzikati na kutoa maamuzi ya kuvunja ndoa ya pande hizo mbili.
Mwanaspoti linafahamu Yanga iliandikiwa barua Mei 4, mwaka juu ikitaka kufahamu hadhi ya mchezaji huyo, vilevile ikitaka kujua imechukua uamuzi gani kuhusu maombi yake ya kuvunja mkataba baada ya kushindwa kumlipa mishahara yake kwa wakati, mazingira magumu ya kufanya kazi na kutommalizia malipo ya ada ya usajili.
TFF iliitaka Yanga itoe majibu hayo ndani ya siku tano tu yaani kutoka siku hiyo hadi jana mchana na Mwanasheria wa Kakolanya, Leonard Richard aliifuata barua hiyo makao makuu ya klabu hiyo na kukuta kila kitu kipo freshi na mteja wake sasa yuko huru.
Mwanaspoti lilimtafuta Mwanasheria huyo ambapo alikiri mchezaji wake kuwa huru kuanzia mchana huo kwani hakuna kipengele chochote kinachombana.
“Kweli kijana kuanzia sasa yupo huru na hapa mkononi nina barua ambayo yeye anatakiwa kuisaini na kuirejesha TFF, tunashukuru Mungu kwa suala hili kumalizika ili kijana aendelea kucheza mpira kwasababu ndio kazi yake,” alisema.
Kakolanya naye alisema; “Ngoja kwanza mpaka jioni nitakujibu hivi sasa naenda kuonana na mwanasheria wangu amenipigia simu, hivyo sifahamu lolote mpaka nikutane naye, lakini naamini hili jambo lishaisha kwa hatua tuliyofikia.”
Kuvunjwa kwa mkataba huo kunamaanisha kipa huyo sasa yupo huru kujiunga na klabu yoyote. Mbali na Simba, Azam FC nayo ilimtaka lakini mambo yalikwama kwa sababu bado alikuwa na makataba Jangwani.

Post a Comment

0 Comments