MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara, Simba na Yanga leo watashuka dimbani kwenye viwanja viwili tofauti kusaka pointi tatu muhimu.
Simba itakuwa kwenye Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam kuikaribisha Kagera Sugar huku Yanga ikiwa kwenye uwanja wa Karume, Musoma dhidi ya wenyeji Biashara United ya Mara.
Hakuna mchezo rahisi hata mmoja, Simba itataka kulipa kisasi kwa Kagera Sugar iliyoifunga mchezo wa raundi ya kwanza mabao 2-1 kwenye uwanja wa Kaitaba Bukoba. Timu hiyo imekuwa ikiisumbua Simba kwani iliwahi kuifunga bao 1-0 kwenye Uwanja wa Taifa, msimu uliopita walipokuwa wakikabidhiwa Kombe la ubingwa mbele ya mgeni rasmi Rais John Magufuli.
Ni wazi wekundu hao awamu hii wanaweza wasikubali kwani wanataka kulipa kisasi kwenye uwanja wao wa nyumbani ambao hawajapoteza mchezo hata mmoja msimu huu. Kingine ni kwamba baada ya kushinda mchezo uliopita wa ligi dhidi ya Coastal Union mabao 8-1 waliishusha Yanga kileleni mwa msimamo wa ligi, hivyo ili kuendelea kubaki juu watapambana kuhakikisha wanapata matokeo mazuri. Simba mpaka sasa imeshacheza michezo 31 na kufikisha pointi 81 huku wapinzani wao Yanga wakicheza michezo 34 na kufikisha pointi 80.
Bado ni vita pande zote mbili zikisaka ushindi katika michezo yao iliyobaki ili kuwa karibu na taji. Kwa upande wa Kagera Sugar itataka kupata matokeo mazuri ili kujinasua kwenye hatari ya kushuka daraja.
Kabla ya michezo ya jana, walikuwa wanashika nafasi ya 12 wakiwa na pointi 40 hazijawahakikishia nafasi ya kubaki. Musoma mchezo wa Yanga na Biashara pia hautakuwa rahisi kwa sababu timu hiyo ya Mara itakuwa mbele ya mashabiki wake ikitaka kushinda na kingine ni kulipiza kisasi baada ya mchezo wa kwanza kufungwa mabao 2-1.
Biashara United inashika nafasi ya 18 ikiwa na pointi 37 hivyo itapambana kupata matokeo mazuri ili kujiondoa ingawa bado haitakuwa kwenye nafasi nzuri. Na Yanga licha ya kuonekana kukataa tamaa katika mbio za ubingwa hawataki kupoteza bali kushinda michezo yao yote iliyobaki. Timu zote kongwe zikishinda kwa maana ya Simba na Yanga uongozi wa ligi utaendelea kubaki kama ulivyo. Na zikipoteza bado watabaki kama walivyo, lakini mmoja akishinda na mwingine kupoteza zinaweza kuachana kwa pointi.
0 Comments