Windows

Kocha Mbeya City atupia zigo wachezaji



KOCHA Mkuu wa Mbeya City, Ramadhan Nsanzurwimo, amesema kitendo cha timu hiyo kufanya vizuri mfululizo kimewafanya wachezaji wake kuridhika na kusababisha wapoteze mechi dhidi ya Yanga.

Juzi Mbeya City walikubali kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Nsanzurwimo, alisema walifungwa bao la kizembe kutokana na makosa yaliyofanywa na wachezaji wake, lakini pia walishindwa kuonyesha jitihada za kurudisha.

“Mchezo ulikuwa wa ushindani lakini maandalizi tuliyofanya haikuwa rahisi kufungwa ila wachezaji walifanya makosa na kuwaruhusu Yanga kufunga,” alisema.

Aidha, alieleza sababu ya wachezaji wake kufanya makosa hayo ni kuridhika hasa kutokana na kupata matokeo mazuri katika michezo iliyopita hivyo kujisahau kuwa wanakutana na timu yenye uzoefu.

“Awali wapinzani wetu Yanga walitushambulia ila kipindi cha pili tulirudisha mashambulizi ingawa wachezaji wangu walionekana kuridhika na bao walilofungwa,” alisema Nsanzurwimo.

Hata hivyo, kocha huyo alisema katika mechi yao ya mwisho atafanya jitihada na kukaa na wachezaji wake ili wasirudie makosa hayo ambayo yanahatarisha uwepo wao kwenye ligi msimu ujao.

Katika msimamo wa ligi hiyo Mbeya City inashika nafasi ya nane ikiwa na pointi 47 baada ya kushuka dimbani mara 37 na kushinda mechi 13, sare nane na kufungwa 16.

Post a Comment

0 Comments