


KOCHA Mkuu wa Biashara United, Amri Said, anapiga hesabu kali ili waweze kuvuna pointi tatu dhidi ya wapinzani wao Simba na kujinasua katika janga la kushuka daraja msimu huu.
Kikosi cha Biashara United kinachoshika nafasi ya 15 katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kikiwa na pointi 43, kinatarajia kukutana na Simba kesho kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Akizungumza na BINGWA jana, Amri alisema nafasi yao ya kubaki Ligi Kuu msimu ujao inategemea matokeo ya mechi mbili zilizobaki ikiwamo ya Simba kutokana na namna msimamo ulivyo.
Alisema kama watavuna pointi tatu mbele ya Wekundu wa Msimbazi watakuwa wamejiweka katika nafasi nzuri ya kubaki msimu ujao.
“Tunautazama kwa jicho tofauti kabisa mchezo dhidi ya Simba kwa sababu tunahitaji pointi tatu muhimu, lakini tumejipanga kupambana kwa hali yoyote kuhakikisha tunaibuka na ushindi,” alieleza Amri.
Aidha, alisema kutokana na hali waliyonayo wamesuka mkakati kabambe wa kujiandaa huku wakijua wanakutana na timu ambayo imeshakuwa bingwa lakini inahitaji kulinda rekodi.



0 Comments