Windows

De Rossi ; Nahodha shupavu anayeacha historia nzito AS Roma



MSIMU huu umekuwa mgumu kwa timu ya AS Roma, ingawa ni jambo linalotegemewa katika mchezo wa soka. Kitu pekee ambacho Waitaliano hao hawakukitarajia ni kuondoka kwa nahodha wao, Daniele De Rossi.

De Rossi ambaye amedumu na ‘Giallorossi’ hao kwa muda wa miaka 18, akiitumikia katika michezo zaidi ya 600, alitangaza kuwa ataiacha klabu yake hiyo ifikapo mwishoni mwa msimu huu huku akiacha rekodi isiyoridhisha.

Ikumbukwe kuwa nahodha huyo aliisaidia timu hiyo kutinga hatua ya nusu fainali Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka jana, lakini hali imekuwa mbaya msimu huu hadi kushuhudiwa kocha wao, Eusebio Di Francesco, akitimuliwa.

Hata hivyo, mambo yalianza kutulia baada ya ujio wa kocha, Claudio Ranieri, ambapo Roma waliweza kucheza mechi saba mfululizo bila kupoteza, lakini matokeo hayo hayakutosha kuipandisha Roma hadi katika nafasi nne za juu.

Zikiwa zimesalia mechi mbili kabla ya kumalizika kwa Ligi Kuu Italia msimu huu, Roma inashikilia nafasi ya sita, pointi tatu nyuma ya Atalanta, lakini wakizidiwa kwa tofauti kubwa ya mabao.

De Rossi ataiacha Roma, lakini hatastaafu soka moja kwa moja kama ilivyokuwa na mkongwe mwenzake, Francesco Totti, ambaye alistaafu mwaka 2017 baada ya kuitumikia Roma kwa muda wa miaka 24.

Kiungo huyo mwenye shughuli pevu dimbani, anatarajia kufikisha umri wa miaka 36 ifikapo Julai mwaka huu, lakini anaonesha kuwa bado ana kitu cha kuendelea kufanya uwanjani.

Licha ya kwamba atakapoiacha Roma na kile cheo cha ‘mchezaji wa timu moja’ hakitamhusu tena De Rossi, lakini mchango wake kwa vigogo hao wa Serie A hautasahaulika kamwe.

Ni sawa na ilivyo kwa watu kama Xavi au Andres Iniesta, walipoondoka Barcelona. De Rossi atabaki kuwa nahodha wa Roma na hatafutika katika mioyo ya mashabiki wa klabu hiyo.

Mkongwe huyo aliibuka kwenye kikosi cha wakubwa Roma muda mfupi baada ya klabu hiyo kutwaa taji lao la mwisho la Serie A mwaka 2001. Alicheza mechi yake ya kwanza Oktoba mwaka huo, mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Anderlecht.

Alianza kutumika mara kwa mara katika kikosi cha kwanza ilipofika mwaka 2003, lakini haikuchukua muda mrefu hadi ilipoonekana kuwa umuhimu wake ni mkubwa ndani ya timu.

De Rossi alianza kutumika katika timu yake ya Taifa ya Italia mwaka 2004 wakati wa michuano ya Mataifa Ulaya kwa vijana chini ya umri wa miaka 21, ambapo walitwaa taji la mashindano hayo.

Baada ya hapo akaanza kupewa majukumu ya kucheza timu ya taifa iliyokuwa chini ya kocha, Marcello Lippi.

Hadi anafanikiwa kutwaa tuzo ya Chipukizi Bora wa Mwaka Serie A (2006), uwezo wa De Rossi, ulishaonekana na kila mtu; kiungo mwenye uwezo mkubwa wa kufanya kazi zote katikati ya uwanja.

Roma na Italia kwa ujumla walivutiwa mno na uwezo wake wa kupokonya mipira na kupiga pasi za kila aina, ingawa hakuwa maarufu sana katika eneo hilo la pasi kama alivyokuwa Andrea Pirlo.

De Rossi anaondoka Roma na kumbukumbu nyingi, mojawapo ni kichapo kikali cha mabao 7-1 walichokipata kutoka kwa Man Utd, Aprili 2007, katika mchezo wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Katika mtanange huo uliowasikitisha mashabiki wa Roma waliosafiri na timu yao hadi kwenye dimba la Old Trafford, De Rossi ndiye aliyefunga bao la kufutia machozi kwa upande wa timu yake.

Mwaka uliofuata, nuksi ya Old Trafford ilimwandama tena De Rossi na safari hii alishindwa kufunga bao kwa penalti na kuipa tiketi Manchester Utd ya kucheza nusu fainali hadi kuwa mabingwa wa UEFA.

Hata hivyo, katikati ya mechi hizo mbili dhidi ya Man Utd, ambazo De Rossi hatapenda kuzikumbuka, Roma ilifanikiwa kunyakua mataji mawili mfululizo ya Coppa Italia.

Misimu mingine ambayo ilikuwa ni mitamu kwa De Rossi, ilikuwa ni 2007/08 na 2008/09, ambapo akiwa chini ya kocha Luciano Spalletti, kiungo huyo aliweza kucheza jumla ya mechi 94 na kufanikiwa kunyakua tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka Serie A (2009).

Kuanzia hapo sasa klabu kadhaa barani Ulaya zikaanza kumuwinda De Rossi. Kuna wakati iliibuka hofu dhidi yake licha ya Roma kumpa mkataba mpya wa miaka mitano ilipofika Ferbuari 2012.

Kwanini walikuwa na hofu kwa De Rossi? Wengi walidhani pengine kiungo wao huyo atashawishika kuondoka na kujaribu kwingineko, japokuwa mkataba mpya ulimfanya awe mchezaji anayelipwa zaidi Serie A.

Klabu kama Man City na Man United zilihusishwa naye, lakini kwa sababu alishaamua kuwa maisha yake yote ni Roma, De Rossi alithibitisha kwamba atabaki kuwa mwana-Giallorossi.

Msimu wa 2013/14, De Rossi na Roma iliyokuwa ikinolewa na kocha, Rudi Garcia, walikaribia kuwa mabingwa wa Serie A kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2001, wakishinda mechi zao 10 za awali.

Hata hivyo, sare mfululizo zilizima ndoto zao na vikafuatia vichapo mfululizo mwishoni mwa msimu kabla ya kujikuta ikimaliza nyuma ya Juventus kwa tofauti ya pointi 17.

Inasikitisha kumwona De Rossi akimaliza miaka yake 18 ya kuitumikia Roma bila taji la Serie A, lakini yeye na Totti watakumbukwa milele na mashabiki wao kutokana na kuithamini na kuiheshimu nembo ya klabu yao.

Kokote atakapoenda, De Rossi, hatasahaulika na watu wa Roma.

Post a Comment

0 Comments