Na John Walter Manyara,
Huduma za afya katika mkoa wa Manyara zinazidi kuboreka kila siku baada ya Serikali kuonyesha jitihada za kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya na Zahanati.
Hayo ameyasema mkuu wa mkoa wa Manyara Alexender Mnyeti akihojiwa na kituo cha redio cha Smile Fm Babati na kueleza kuwa katika mkoa wake vituo vya Afya vinazidi kuongezeka ambapo Rais John Pombe Magufuli alitoa shilingi milioni 500 kwa ajili ya kuongeza Zahanati katika vijiji na kata pamoja na shilingi Milioni 400 za kufanyia marekebisho vilivyopo.
Ametolea Mfano kituo cha Afya Simbay kilichopo Hanang, Mbulu Tlawi na kituo cha Afya Daudi ambavyo vina muonekano wa hospitali ya wilaya.
"Katika mkoa wetu tuna hospitali ya rufaa ambayo inafanya vizuri na wilaya zote tuna hospitali"alisema Mnyeti
Aidha Rc Mnyeti amesema Serikali imeshatoa pesa kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya wilaya ya Mbulu vijijini itakayojengwa Dongobesh.
Mnyeti ameipongeza serikali kwa kuonyesha nia ya kuwapa wananchi huduma nzuri za afya kwa kuongeza bajeti katika wizara ya afya kutoka shilingi bilioni 60 miaka ya nyuma hadi kufikia shilingi bilioni 268 ongezeko mara tatu zaidi.
Amesema katika mkoa wa Manyara kuanzia vituo vya Afya,Zahanati na Hospitali zote upatikanaji wa dawa ni asilimia 100 dawa zote za msingi zinapatikana.
0 Comments