Na Thabit Madai, Zanzibar
SERIKALI ya mapinduzi ya Zanzibar imewaomba wadau wa elimu nchini kuendelea kushirikiana kwa pamoja kwa lengo la kuimarisha sekta ya elimu kwa maendeleo ya watu wake.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya chakula kwa ajili ya kambi ya maandalizi ya mitihani ya kidato cha sita kwa wanafunzi wa skuli ya Lumumba kilichotolewa na kampuni ya Jendele Technology Solution (JTS), Mkuu wa mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud, alieleza kuwa kufanya hivyo kutachochea kasi ya maendeleo ya sekta hiyo na jamii kwa ujumla.
Alisema ili kufikia maendeleo ya kweli, ipo haja ya kila mmoja miongoni mwa jamii kutoa mchango bila ya kujali dhamana au nafasi aliyonayo.
Alieleza kuwa serikali itaendelea kuipa kipaumbele sekta ya elimu kwa kujenga miundombinu, kusomesha walimu na kugharamia mchakato wa utoaji wa elimu ili kupanua wigo wa upatikanaji wa elimu.
Mkuu huyo wa mkoa aliupongeza uongozi wa taasisi hiyo kwa uamuzi wao wa kuchangia wanafunzi hao wanaotarajiwa kufanya mitihani ya kuhitimu elimu ya sekondari ya juu baadae mwaka huu kwani kufanya hivyo kutawaongezea ari ya kujifunza wanafunzi hao na kuwafanya wajiandae vyema na mitihani yao.
Aidha aliwataka wanafunzi hao kuutumia vyema msaada uliotolewa kwa kujiandaa kikamilifu na mitihani yao kwa kuzingatia vyema mafundisho ya walimu wao na kujiepusha na mambo yasiyoendena na elimu.
Awali akikabidhi msaada huo Mkurugenzi Mtendaji wa JTS, Omar Vuai Shein alieleza kuwa uamuzi huo umetokana na kuvutiwa na juhudi zinazochukuliwa na walimu wa skuli hiyo.
Alisema maendeleo ya sayansi na teknolojia yanahitaji mazingira bora ya kujifunzia, hivyo taasisi yake itaendelea kuisaidia sekta ya elimu ili kupata wataalamu watakaochangia uchumi wa taifa.
Alisema JTS kama taasisi inayojihusisha na masuala ya teknolojia, imeona haja ya kutoa mchango wake na kuwahimiza wanafuzi kujikita katika masomo ya sayansi ili taifa liwe na wataalamu wengi wazalendo.
Nae Mwalimu Mkuu wa skuli ya Lumumba Mussa Ali Mussa alieleza kuwa wameanza kambi mapema kutokana na maombi ya wanafunzi na wazazi wa wanafunzi hao ambao walikubali kuichangia kambi.
0 Comments