Windows

Aussems- Refa hakutenda haki







LICHA ya Simba kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mbeya City juzi, Kocha wake, Patrick Aussems amesema hajaridhishwa na maamuzi ya mchezo huo.

Katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, wekundu hao walitangulia kufungwa kipindi cha kwanza, kisha wao kusawazisha na kupata bao la ushindi kipindi cha pili.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Aussems amesema tangu wapate penalti mbili katika moja ya mchezo uliopita dhidi ya KMC ambazo zililalamikiwa, waamuzi wamekuwa hawatoi tena nafasi hizo kwenye sehemu walikostahili.

“Leo (juzi) sina furaha na maamuzi kwa sababu kuna sehemu hatukutendewa haki,”alisema na kuongeza kuwa jambo la muhimu wanashukuru kwasababu wamepata pointi tatu.

Kocha huyo aliwapongeza wachezaji wake kwa kuendelea kucheza kwa kujitolea akisema wamekuwa mashujaa wasiokata tamaa.

“Wachezaji wameendelea kuonyesha kiwango bora, wanacheza kwa kujitoa bila kukata tamaa, najivunia ubora wao wa hali ya juu,”alisema Aussems.

Simba inatarajia kucheza mchezo mwingine leo dhidi ya Tanzania Prisons utakaochezwa huko Mbeya.

Kwa upande wake, Kocha wa Mbeya City Ramadhan Nswanzirimo naye pia, ametoa lawama hasa kwa kocha msaidizi namba moja wa mchezo huo akisema hakuwa sahihi katika baadhi ya maamuzi.

Alisema sio kwamba Simba haikustahili kushinda isipokuwa faulo wanazopewa nyingine sio sahihi kwao kwasababu inawatengeneza nafasi ya kufunga.

“Sijafurahishwa kwasababu hatukustahili kupoteza mchezo ila waamuzi ndio wenye kuamua matokeo ya mchezo, walitoa faulo kwa Simba ambayo haikustahili,”amesema huku akiongeza anawapongeza wekundu hao kwa kushinda.

Nswanzirimo alisema kinachoonekana mpira wa sasa unaendeshwa kwa pesa hivyo, timu yenye pesa ndio iliyoshinda.

Post a Comment

0 Comments